Hali ya Uchumi ni Mbaya- Zitto Kabwe

Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amefunguka na kusema kuwa uchumi wa nchi unazidi kudidimia na thamani ya shilingi inazidi kushuka huku mfumuko wa bei ukizidi kupaa.

Zitto Kabwe anasema kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambayo jana ametoa taarifa yake juu ya hali ya uchumi nchini ni kwamba hali si nzuri kwani uchumi umeonyesha kusinyaa na kudidimia huku wananchi wa hali ya chini wakiwa wahanga wakubwa zaidi.

"Taarifa hiyo inaonyesha namna hali ya uchumi wetu inavyozidi kuwa mbaya zaidi kwa wananchi wa hali ya chini , kwa mfumuko wa bei umepanda mno tangu kuanza kwa utekelezaji wa bajeti ya 2017/18, ongezeko ambalo limechangiwa zaidi na kupanda kwa bei ya bidhaa za chakula (bidhaa ambazo wananchi wengi zaidi wanazitumia)" alisema Zitto Kabawe

Aidha Zitto Kabwe amedai kushuka kwa thamani ya sarafu ya Tanzania kumezidi kuongeza maumivu kwa wananchi na ili kusaidia kupunguza ukali na gharama za maisha mishahara ilipaswa kupanda kwa asilimia 8 zaidi.

"Thamani ya sarafu ya Tanzania imeshuka, uwezo wa Tsh. 100 kununua bidhaa umeshuka hadi Tsh. 92.18. Maana yake ni kuwa mwaka 2016 shilingi 100,000 ilikupa bidhaa za shilingi 100,000. Mwaka huu 2017 shilingi 100,000 inakupa bidhaa za shilingi 92,000. Kwa hiyo ili upate bidhaa za shilingi laki moja inakubidi uongeze shilingi elfu 8 zaidi. Kiuchumi, ili kulinda hali za wananchi, mishahara ilipaswa kupanda kwa asilimia 8 ili kuwapunguzia maumivu ya gharama za maisha. Lakini hali hiyo inatokea katika wakati ambao mishahara haijapanda, na Rais wa nchi yetu kasema Serikali anayoingoza haitapandisha kabisa mishahara. Hali ni mbaya mno mtaani, mijini uzalishaji wa bidhaa za viwanda umeshuka kwa zaidi ya nusu, kutoka trilioni 1.5 mpaka bilioni 700 tu" alisisitiza Zitto Kabwe

Mbali na hilo Zitto Kabwe ametoa ushauri wa nini serikali inapaswa kufanya ili kukabiliana na hali hiyo na kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi, Zitto amedai Serikali inapaswa itazame namna inatekeleza mipango yake ya Maendeleo, Serikali isikilize na kufanyia kazi mawazo ya sekta binafsi katika kuweka sawa mazingira ya uwekezaji bila kupoka haki ya nchi kufaidi na rasilimali zake na pia ameitaka serikali ifanyie kazi haswa uchumi wa vijijini kwa kurekebisha mapungufu yote yanayoshusha uzalishaji kwenye sekta ya kilimo.

from UDAKU SPECIAL
Soma Zaidi

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini