Mawaziri wa Maji wa Nchi za Bonde la Mto Nile kukutana Uganda

                                                                           

Na.Mwandishi Wetu- MAELEZO.

Mkutano wa 25 wa mwaka wa Mawaziri wa maji kutoka katika nchi za Bonde la Mto Nile unatarajiwa kufanyika Oktoba 12, mwaka huu Mjini Entebe nchini Uganda lengo ikiwa ni kujadiliana na kupitisha maamuzi muhimu pamoja na mkakati wa miaka 10 wa ushirikiano na uendelezaji wa Bonde hilo.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mradi wa pamoja wa kuendeleza Bonde la Mto Nile na nakala yake kupatikana Jijini Dar es salaam, Mawaziri hao watajadiliana juu ya changamoto zinazolikabili bonde la Mto Nile pamoja na jinsi ya kukabiliana nazo.

 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mambo mengine yatakayojadiliwa ni ufuaji wa umeme kwa kutumia maji pamoja na biashara ya nishati ya umeme, kuongezwa kwa usalama wa chakula, uhifadhi na ulinzi wa vyanzo vya maji, kuongeza nguvu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuimarisha usimamizi wa maji katika Bonde la Mto Nile kwa nchi wanachama, pamoja na usimamizi endelevu wa Rasilimali za mto huo.

 

 

 Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa, mambo mengine yatakayojadiliwa na Mawaziri katika mkutano huo ni kuhusu sektretarieti ya Bonde la Mto Nile, pamoja na kupitia mpango kazi wa mwaka wa fedha wa 2017 hadi 2018.

 

Mkutano huo utashuhudia pia mabadiliko ya uongozi wa juu wa Baraza la Mawaziri wa maji wa nchi za Bonde la mto Nile, hii ni kotokana na utaratibu mradi huo uliojiwekea wa kubadilishana uenyekiti kila mwaka kutoka nchi moja kwenda nyingine.

 

Mkutano huo utafanyika kwenye hoteli ya Imperial Resort Beach mjini Entebe, na utahudhuriwa na mawaziri wa maji wa nchi wanachama ambazo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Tanzania, Sudani Kusini pamoja na wenyeji Uganda.

 

Wengine watakaohudhuria katika mkutano huo ni wajumbe wa kamati ya utendaji ya Bonde la Mto Nile, wabia wa maendeleo asasi za kiraia pamoja na waandishi wa habari.

 

Mradi wa kuendeleza Bonde la Mto Nile ni mradi wa uhusiano wa kikanda kwa nchi wanachama wa ulioanzishwa Februari 22, 1999 mahsusi kwaajili ya kuenderleza na kusimamia Rasilimali ya Bonde la mto Nile.


Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini