Waziri Kairuki Aweka Wazi Vipaumbele vyake

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ameeleza vipaumbele  vyake katika Wizara kuwa ni pamoja na  udhibiti wa utoroshaji wa madini nchini, maslahi kwa wafanyakazi huku akiwataka watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu.

Kairuki ameyasema hayo mapema leo tarehe 10 Oktoba, 2017 jijini Dar es Salaam  alipozungumza na  watumishi wa Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake, waliopo Dar es Salaam na Makao Makuu  ya Wizara Dodoma. Lengo La kikao hicho lilikuwa ni kufahamiana na kupanga mikakati  ya kushirikiana ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa Uchumi wa nchi.

Taasisi zilizoshiriki katika kikao hicho ni pamoja na  Wakala wa Jiolojia  Tanzania (GST), Shirika la Madini la  Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI) pamoja na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini na Mpango wa Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (TEITI).

Amesema kuwa Sekta ya Madini  inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwataka wataalam wa madini kubuni mbinu za ukusanyaji wa maduhuli pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye uchimbaji madini.

Katika hatua nyingine aliwataka wataalam hao kubuni mikakati  ya kuzuia utoroshaji wa madini nchini ili nchi ipate mapato stahiki.Amewataka watumishi kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na kuwa wabunifu ili  sekta hiyo iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Naye Naibu  Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewakumbusha  watumishi kuzingatia Dira na Dhima ya Wizara  ikiwemo kufanya kazi kwa tija ili hatimaye  sekta ya madini iweze kuchangia katika uchumi wa nchi kwa kuwa mchango wa sekta husika bado ni kidogo.

from UDAKU SPECIAL
Soma Zaidi

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini