Huyu ndiye Pierre Lechantre..kocha bora wa Afrika na Asia

KOCHA Mkuu mpya wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre, amekishuhudia kikosi chake kikiibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Singida United katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Katika ushindi huo uliochangiwa na Mganda Emmanuel Okwi aliyetokea benchi na kutupia mawili katika kipindi cha pili, Simba ilicheza kwa kujiamini zaidi ya wageni hao.

Lechantre, ambaye alitangazwa rasmi jana kuwa Kocha Mkuu wa Simba, ni wa kiwango cha juu, na haijawahi kutokea kwa klabu za hapa nchini kunasa kocha wa kiwango hicho katika kipindi cha hivi karibuni, imefahamika.

Lechantre ambaye aliwasili nchini juzi usiku na kuanza mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo ambayo jana mchana yalifikia tamati baada ya kukubaliana, sasa anazima tetesi za majina kibao ya makocha waliokuwa wakihusishwa kupewa mikoba ya Mcameroon Joseph Omog.

Moja ya sifa kubwa ya kocha huyo katika kipindi cha hivi karibuni ni pamoja na kuinoa timu ya Taifa ya Congo mwaka 2016, ambayo imekata tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika Urusi baadaye mwaka huu, na sasa amepewa mikoba ya kuiongoza Simba baada ya viongozi wa klabu hiyo kuamua kuachana na Mbrazil Fabio Lopez, aliyeko nchini tangu Jumanne.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema Lechantre atasaidiwa na Mrundi Masoud Djuma, ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo baada ya kuondoka kwa Omog.

Manara alisema Lechantre amefuatana na kocha wa viungo, Mohammed Aymen, raia wa Morocco na baada ya kufikia makubaliano, wanatarajia kukamilisha taratibu za kupata kibali na hatimaye Mfaransa huyo aweze kuanza kazi yake mapema.

Sifa nyingine ya Lechantre, ni kwamba analifahamu vema soka la Afrika, kwani aliwahi kuiongoza Cameroon kuchukua ubingwa wa Afrika mwaka 2000 huku klabu alizowahi kuzifundisha ni pamoja na Al Ittihad ya Libya, Al Arabi (Qatar), CS Sfaxien na Club Africaine zote za Tunisia.

Mbali na kuiongoza Simba kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara ambalo linashikiliwa na Yanga, Mfaransa huyo atatakiwa kuhakikisha ‘Wekundu wa Msimbazi’ hao wanaodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, wanafanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika yatakayoanza mapema mwezi ujao.

Mechi Taifa Mabao ya Simba katika mechi ya jana yalifungwa na Shiza Kichuya katika dakika ya tatu huku la pili likiwekwa kimiani na Asante Kwasi katika dakika ya 23 likiwa ni bao lake la kwanza kwa Simba iliyomsajili kwenye dirisha dogo lakini la sita kwake msimu huu.

Okwi aliifungia Simba mabao mawili moja katika dakika ya 75 na la nne likiwa ni dakika ya 82 na kuwanyamazisha mashabiki wa Singida United waliokuwa wanaishangilia timu hiyo.

Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 29 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 27 ambayo jana ilipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Majimaji waliokuwa wenyeji katika mchezo uliofanyika mapema mchana.

Mtibwa Sugar wenye pointi 24 wako katika nafasi ya tatu wakifuatiwa na Singida United yenye pointi 22 wakati mabingwa watetezi, Yanga wakiwa watano baada ya juzi kufikisha pointi 22.

Vinara hao wa Ligi Kuu wanatarajia kuondoka jijini leo kuelekea Kagera kwa ajili ya kuwavaa wenyeji wao Kagera Sugar katika mchezo utakaopigwa Jumatatu Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

The post Huyu ndiye Pierre Lechantre..kocha bora wa Afrika na Asia appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini