JPM apigilia msumari usajili wa meli mpya nchini

Rais John Magufuli ameagiza kusitishwa usajili wa meli mpya hapa nchini kufuatia taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya na bidhaa nyingine zinazopingwa na kimataifa katika meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania ambazo hadi sasa zimefikia tano.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo jana Ijumaa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume.

Pia amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo na kuhakikisha jina la Tanzania halichafuliwi ndani na nje ya nchi.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imeeleza kuwa maagizo hiyo yalitolewa wakati Rais akifanya mazungumzo na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) ambapo mawaziri hao nao walikuwepo.

“Kafanyeni uchunguzi wa kina kwa meli zote zinazopeperusha bendera ya Tanzania, fanyeni uchunguzi kwa meli zilizokamatwa ambazo ni tano na pia hizi 470 zilizosajiliwa na zinaendelea kufanya kazi zichunguzeni, hatuwezi kuacha jina la nchi yetu lichafuliwe na watu wanaofanya mambo kwa masilahi yao,” alisema Rais Magufuli.

Pia, Rais Magufuli amehimiza kutekelezwa kwa maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu juzi, ambaye alitangaza kuzifutia usajili wa meli mbili zilizokamatwa sanjari na kuamuliwa kushusha bendera ya Tanzania.

Suluhu alizitajia meli hizo kuwa ni Kaluba yenye usajili wa namba IMO6828753 iliyokamatwa maeneo ya Jamhuri ya Dominican Desemba 27 mwaka jana ikiwa na wastani wa tani 1.6 ya dawa za kulevya pamoja na Andromeda yenye namba za usajili IMO 7614666 iliyokamatwa ikisafirisha silaha kinyume na sheria za kimataifa.

The post JPM apigilia msumari usajili wa meli mpya nchini appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini