Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa ukuta wa bahari Kigamboni wenye urefu wa mita 500.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa ameketi kwenye moja ya sehemu za kupumzikia pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.January Makamba(kulia) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa dar es Salaam Mhe. Paul Makonda wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa ukuta wa bahari Kigamboni wenye urefu wa mita 500.
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuchana na vitendo vya uharibifu wa mazingira kwa lengo la kujiepusha na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.
Mama Samia amesema hayo leo jijijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya ujenzi wa kuta za kingo katika Bahari ya Hindi eneo la Ocean Road na Kigamboni.
Amesema kuwa Tanzania imeharibu mazingira yake kwa kiasi kikubwa hali inayofanya sehemu kubwa ya maeneo yote kuwa na hali tofauti na tulivyotegemea.Ametoa mfano Mji wa Dodoma ambao watu wamekata miti yote na hivyo kusababisha eneo hilo kuwa jangwa kiasi cha kusababisha maafa pindi mvua zinaponyesha.
Ametaja kuwa mikoa mingi ambayo iliyokuwa na baridi sasa hivi imekuwa ikiongoza kwa joto sawasawa na mikoa iliyopo Pwani kwa mfano mikoa ya Kilimanjaro kila ukiangalia utabiri wa hali ya hewa unaambiwa ina nyuzi joto 32 hadi 33, kiasi ambacho awali haikuwahi kufikia hapo. Amesema adhabu yote hiyo na athari zinazoonekana sasa inatokana na uharibifu huo mkubwa wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wanachi kwenye maeneo mbalimbali nchini .
“Napenda kutumia mfano anaotumia Papa Francis kuwa ukimkosea mwanadamu utakwenda kulia kanisani au Msikitini utasamehewa lakini ukiyakosea mazingira hayana Msikiti wala Kanisa yatakuadhibu mpaka utakaporudi kuwa rafiki tena,"amesema Makamu wa Rais .
Ameongeza kuwa "Nasi tumeharibu mazingira kwa kukata miti, kuchimba mchanga katika fukwe na matokeo yake bahari imepata nguvu ya kula ardhi yetu,hivyo turekebishe tulipoharibu ili kurudisha urafiki huu".Amesema kwa Mkoa wa Dar es Salaam wakazi wake wamekuwa wakitupa taka katika mitaro na ikiziba inaleta madhara ya mafuriko, hivyo hiyo ni hasara kwa Taifa kwa kuwa tunatumia muda mwingi kutoa pole na anayepewa pole hutegemea uende na chochote umsaidie kama mahindi na fedha.
Amefafanua baada ya kutembelea miradi mbalimbali keshokutwa atakutana na wadau wa mazingira wa Dar es Salaam kupanga mikakati ya kuokoa mazingira.Kwa upande wa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira January Makamba amesema pamoja na kuwa Tanzania haichangii kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira lakini ni wahanga wa athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Athari hizi zinaathiri moja kwa moja uchumi wa nchi kutokana na kuathirika kwa kilimo, utalii na uvuvi, hivyo tunaendelea na miradi mbalimbali ya kukabiliana na hali hiyo ikiwamo ujenzi wa kingo za bahari maeneo mbalimbali,” amesema.Wakati huohuo Mtaalamu wa miradi kutoka wizara hiyo,Fred Manyika amesema miradi hiyo inayofadhiliwa na mfuko wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi(Adoptation Fund) inagharimu dola za Marekani Milioni 5.8.
“Fedha hizi zimefanya ujenzi wa ukuta wa kingo za bahari katika eneo la kigamboni na ule wa jirani na Ocean Road jijini hapa,” amesema Manyika.Ameongeza kuwa miradi mingine inajengwa katika Manispaa za Ilala na Temeke jijini Dar es Salaam inayogharimu dola za Marekani 900,000.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments