Tendaguru: Mjusi wa Tanzania anayepamba makumbusho Ujerumani

UNAPOINGIA ndani ya makumbusho ya viumbe hai ya Berlin, Ujerumani, unakutana na ukumbi wenye masalia ya viumbe vilivyoumbwa kwa maumbo yake ya asili. Kwa mtu ambaye hajaambiwa viumbe hao ni nini, akimuona mmojawapo ambaye ni mkubwa, anaweza kudhani ni twiga kwa maana ya kuangalia umbile la shingo na miguu.


Lakini hatamfananisha na twiga moja kwa moja kwa kuwa kiumbe huyo ambaye mifupa ndiyo inamtambulisha, ni mkubwa sana na mrefu zaidi ya twiga. Ni kiumbe mkubwa kuliko hata tembo ambaye ndiye anaaminika kuwa mnyama mwenye umbo kubwa kupita wanyamapori wote kwa kuwa na uzito mkubwa pia. Tembo anakadiriwa kuwa na uzito wa tani mbili hadi tano; lakini haoni ndani kwa viumbe hawa wanaopamba ukumbi mmojawapo wa makumbusho hayo.
Ili kumfikia kiumbe huyu kwa uzito, inapaswa kuunganisha tembo 10 wenye uzito wa tani tano. Huyo siyo mwingine bali ni mjusi mkubwa aliyevumbuliwa katika eneo la Tendaguru mkoani Lindi miaka 100 iliyopita. Mjusi huyo mkubwa ambaye ni pambo na kivutio kimojawapo kwenye makumbusho hayo ya Berlin, Ujerumani, ana uzito wa tani 50.
Mjusi huyo mkubwa sana na wengine sita wadogo (ambao siyo halisi) na ambao kwa jina la kitaalamu wanajulikana kama ‘dinosaurs’, masalia yao yaligunduliwa katika eneo la Tendaguru. Masalia hayo yalikusanywa na kupelekwa Ujerumani ambako wataalamu waliyaunda na kisha kuyaweka kwenye makumbusho haya yaliyojengwa tangu mwaka 1889.
Tendaguru ndilo jina ambalo machapisho katika makumbusho hayo na hata wataalamu na watafiti wanalitumia kutambulisha mijusi wote wakubwa, siyo tu hao wa Tanzania, bali pia wanaotoka nchi nyingine. Anakadiriwa kuwa na umri wa miaka milioni 150. Ana urefu wa meta 13.7 kwenda juu huku akikadiriwa alikuwa na moyo wenye kilo 400 na chakula chake kilikuwa mimea.
Akielezea historia ya mjusi huyo, mwanasayansi, mtaalamu na mtafiti wa mambo ya kale katika makumbusho hayo, Dk Daniela Schliart anasema aligunduliwa kati ya mwaka 1907 na 1909. Anasema wanasayansi waliogundua mjusi huyo walikuwa wametumwa na makumbusho hayo kutafuta madini ndipo wakakumbana na masalia hayo. Walianza kuchimba katika kilima hicho cha Tendaguru, wakakusanya mabaki ambayo yalisafirishwa hadi Ujerumani.
Mjusi huyo anayeshikilia rekodi duniani katika kitabu cha Guinness kama mjusi mkubwa zaidi duniani, baada ya mabaki kufikishwa Ujerumani, wataalamu waliunganisha masalia na iliwachukua miaka 20 kupata mwonekano kamili wa mjusi huyo mkubwa duniani. Kwa mujibu wa Dk Schliart, sehemu za mjusi zenye masalia halisi ni miguu, mkia, mbavu na shingo.
Wanasayansi na watafiti hawa wa mambo ya kale wanaeleza kuwa, katika utafiti wao walibaini kuwapo aina 13 tofauti za mijusi ambao baadhi waliishi kwa kula nyama na wengine wakila mimea. Ndani ya makumbusho hayo, lipo eneo maalumu linaloonesha mfano wa kilima cha Tendaguru na namna ambavyo watafiti walivyokutana na masalia hayo na kuanza kuyachimba.
Ipo ramani ya Tanganyika (Tanzania) inayoonesha eneo la Tendaguru lilipo na pia vikioneshwa vifaa halisi vya uchimbaji vilivyotumika enzi hizo kuchimba masalia hayo. Vifaa hivyo ni pamoja na sururu na koleo ambazo zilitumika kuchimbua masalia hayo. Aidha, katika eneo hilo zimewekwa chupa za dawa za binadamu pamoja na sindano ambazo watafiti hao walikwenda nazo Tanzania kwa ajili ya kujihami na maambukizi ya malaria.
“Siyo kwamba huyu mjusi alikutwa akiwa amekamilika; bali baada ya watafiti kubaini mabaki, waliyachimba na kupata sehemu mbalimbali ambazo zilikuja kuunganishwa huku Ujerumani,” anasema Dk Schliart. Mtafiti huyu anaeleza namna walivyobaini umri wa mjusi huyo na kusema ni kwa kuangalia makundi ya madini yalivyopangiliwa na pia kwa kutumia programu za kompyuta.
Mjusi huyu ambaye amekuwa akisababisha mijadala nchini hususani miongoni mwa wabunge wakitaka arejeshwe, wataalamu katika makumbusho wanaeleza kuwa anahitaji kutunzwa kwa uangalifu. Miongoni mwa matunzo hayo kwa mujibu wa wataalamu, ni pamoja na kutumia kemikali maalumu za kumlinda asije kusambaratika.
Hata hivyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Sayansi, Dk Christoph Hauser anasema wangependa kushirikiana na Tanzania katika utaalamu wa uchimbaji na uhifadhi wa malikale kama ilivyo kwa huyo mjusi.
Katika maelezo yake kwa Watanzania waliofika kwenye makumbusho hayo wakiongozwa na Mbunge wa Muleba Kusini, Dk Hauser anasema ushirikiano huo uwe wa kutayarisha Watanzania kwa ajili ya uchimbaji wa masalia mengine ya mijusi kwani inaaminika bado wapo mijusi wengine katike eneo hilo la Tendaguru.
Anasema ni lazima watayarishe wataalamu wa kutunza masalia hayo ya mijusi kwa sababu imekaa miaka mingi, hivyo inaweza kuharibika. Alionesha kemikali ambazo wanatumia kuhakikisha kwamba masalia haya yaliyounganishwa hayasambaratiki.
Dk Schliart anasema wanaamini kwamba bado kuna mijusi wengine katika eneo la Tendaguru, hatua inayohitaji kuwa na wataalamu nchini kwa ajili ya utafiti zaidi wa kuwapata na kuwahifadhi nchini. Kwa upande wake, Profesa Tibaijuka anaahidi kuzungumza na viongozi wa serikali na wahusika wengine kuona ni namna gani ushirikiano huo utakuwa.
Anamshukuru Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi aliyefanya maandalizi ya ujumbe huo wa Watanzania kutembelea makumbusho hayo kujionea mjusi huyo ambaye ni nembo ya taifa.
“Kwa kweli ni kitu kikubwa sana na mjusi huyu tunajivunia ni nembo ya taifa letu... Kwa sasa hivi, mimi nafikiri cha msingi ni kwamba mjusi yupo, taratibu za kumpeleka nyumbani nadhani ni kitu kizuri sana; ni kitu cha kujivunia lakini kinataka matayarisho,” anasema Profesa Tibaijuka.
Akirejea hoja ambazo zimewahi kutolewa bungeni na baadhi ya wabunge wakishinikiza serikali imrejeshe mjusi nchini, Tibaijuka anasema, “Kwa hiyo mimi nafikiri kwamba hayo yote yapo sahihi, lakini sasa siyo tukio, ni mchakato kwa hiyo lazima tujitayarishe.” Hoja za kutaka mjusi huyo kurejeshwa nchini siyo za wabunge pekee bali pia watu mbalimbali kupitia majukwaa kama vile mitandao ya kijamii wakiamini kwamba kwa njia hiyo mapato yake yataonekana.
Wapo ambao wamewahi kutaka faida inayotokana na mjusi huyo igawanywe pia kwa Tanzania. Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Sayansi, Dk Hauser anafafanua kuwa makumbusho hayo si kwa ajili ya mjusi wa Tanzania pekee, bali yana masalia ya viumbe wengine kama vile nyoka, ndege, simba, chui na mijusi wakubwa kutoka nchi mbalimbali.
Anaonesha mjusi mwingine aliyeletwa mwaka juzi kutoka Montana, Marekani ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 66 mwenye uzito wa tani nane ambazo ni kidogo ikilinganishwa na Tendaguru mwenye tani 50. Akielezea hoja juu ya mapato, Dk Hauser anasema sehemu kubwa ya bajeti ya makumbusho na kituo hicho cha utafiti inatoka serikalini na ni euro milioni 15 kwa mwaka.
Makumbusho hayo yaliyo chini ya Wizara ya Elimu na Utafiti ambayo huingiza wastani wa watu 500,000 kwa mwaka, kiingilio chake kwa sasa ni euro nane kwa kila mtu isipokuwa wenye zaidi ya umri wa miaka 65 ambao wanalipa euro tano.
“Hakuna makusanyo makubwa tunayopata kutokana na kiingilio. Hii ndiyo makumbusho yenye viwango vidogo vya tozo ya kiingilio ukilinganisha na makumbusho nyingine,” anasema Hauser. Kwa mujibu wa wataalamu hao, watafiti kutoka kituo hicho wamekuwa wakienda maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutafiti na kukusanya sampuli za kiutafiti za mambo ya kale.
Maelezo ya Dk Hauser na uhalisia wa makumbusho hayo, yanashabihiana na yaliyotolewa Bungeni Juni mwaka huu na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani.
Akijibu hoja kuwa serikali inapunjwa mapato yatokanayo na viingilio katika makumbusho hayo, Makani (ambaye sasa si waziri) alisema ni ngumu kufahamu kiasi kinachopatikana kama kiingilio kwa ajili ya kuwaona mijusi wa Tanzania .
Aliwaeleza wabunge kuwa makumbusho hayo yana kumbi nyingi zenye masalia kutoka nchi mbalimbali na gharama za kuyaendesha hutolewa na Serikali ya Ujerumani. Bunge lilielezwa kwamba, kutokana na majadiliano ya kina yanayohusisha wataalamu wabobezi katika masuala ya malikale kutoka Tanzania na Ujerumani, imekubalika kuwa serikali itaendesha shughuli za utafiti zaidi huko Tendaguru na katika maeneo jirani ili kuwezesha uchimbaji wa mabaki ya mijusi wengine.

Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini