Hukumu ya Papii Kocha na Babu Seya Kusomwa Arusha

Hukumu ya Papii Kocha na Babu Seya Kusomwa Arusha
Mahakama ya Afrika ya watu na haki za binadamu yenye makao yake makuu jijini Arusha, leo inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya mwanamuziki nguli nchini, Nguza Viking na mwanawe Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ waliyokuwa wameifungua katika mahakama hiyo dhidi ya serikali.


Nguza na mwanawe walifikisha malalamiko yao mbele ya mahakama hiyo wakidai kunyimwa haki za msingi katika mahakama za Tanzania na kuomba mahakama hiyo ya Afrika kuamuru kuachiliwa. Juni 2004, Nguza na mwanawe Johnson walitiwa hatiani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuhukumiwa kufungwa jela maisha, baada ya kukutwa na hatia ya kunajisi na kulawiti watoto wadogo 10 .

Wasanii hao kwa sasa wako uraiani baada ya kutoka kwa msamaha wa Rais John Magufuli, Desemba mwaka jana. Katika maombi yao waliyowasilisha katika Mahakama ya Afrika, walalamikaji waliiomba mahakama hiyo kutoa uamuzi kwamba haki zao zilivunjwa na hivyo waachiwe huru na kulipwa fidia.

Walidai katika hati yao ya maombi mbele ya Mahakama ya Afrika kuwa walipokamatwa mara ya kwanza hawakupewa haki ya kuelezwa sababu za kukamatwa kwao, kinyume na mkataba wa haki za binadamu kifungu namba 1,2,3,5,7(1)b),13 na 18 ambapo baada ya kukamatwa waliwekwa kizuizini bila ya kuwasiliana na mwanasheria wao au mtu mwingine yeyote.

Pia walilalamika wakiwa ndani ya mahabusu, Polisi waliwatesa kinyume na haki za binadamu na baada ya kushikiliwa kwa siku nne ndio walielezwa kuwa walikamatwa kwa makosa ya kunajisi na kulawiti, jambo ambalo walilikana.

Aidha walidai kuwa mahakama haikuwatendea haki ikiwemo kutupilia mbali maombi ya kuwasilisha ushahidi wa vipimo vya damu na mkojo katika utetezi wao dhidi ya kesi hiyo iliyokuwa ikiwakabili.

Pia walidai wanaodai kuambukizwa virusi vya Ukimwi (HIV) na kisonono walidanganya mahakama kwa kuwa mdaiwa wa kwanza alikuwa hanithi na aliomba kupimwa hali yake ya uhanithi na kwamba hawezi kufanya vitendo vya ngono lakini maombi yake yalitupiliwa mbali na mahakama.

Walidai pia kuwa mahakama iliyowahukumu haikuzingatia kuwa wazazi wa watoto waliodaiwa kunajisiwa na kulawitiwa walikuwa wakifahamu nyumba waliyokuwa wakiishi na walikuwa wakitembelea eneo hilo mara kwa mara hivyo kujua chumba walichokuwa wakiishi.

Kwa mujibu wa Nguza na mwanawe ushahidi uliokuwa ukitolewa haukuwa wa haki, ikiwemo hata mashtaka yao yaliyowasilishwa mahakamani hapo yalikosea tarehe ya siku tuhuma za makosa yalipodaiwa kufanyw,a jambo ambalo walishindwa kuandaa ushahidi.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini