MFANYABIASHARA Hariri Mohammed (45) mkazi wa wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na tuhuma za kusafirisha zaidi ya gramu 214 za madawa ya kulevya.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Clara Chalwe, mbele ya hakimu mkazi mkuu, Huruma Shahidi, alidai kuwa Machi 2 mwaka huu katika eneo la Matitu, katika wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa alisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine Hydrochloride zenye uzito wa gramu 214.11.
Baada ya kusomewa hati ya mashtaka mtuhumiwa hakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za dawa za kulevya isipokuwa kwa kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hivyo, upande wa mashtaka umeiambia mahakama kwamba upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo kesi imeahirishwa hadi Aprili 4 mwaka huu.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments