Ni bajeti ya kupaa kimaendeleo

SERIKALI imesoma makadirio ya mwelekeo wa bajeti ya Sh trilioni 32.476, ambazo zinatarajiwa kukusanywa na kutumiwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019, ikiwa na ongezeko la Sh bilioni 764, ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2017/18.

Katika mwaka 2017/18, serikali ilipanga kukusanya na kutumia Sh trilioni 31.712, ambapo serikali iliweza kutoa mgawo wa Sh trilioni 17.402 kwa mafungu mbalimbali, ambayo ni asilimia 85 ya makadirio ya bajeti hadi Januari mwaka huu.

Kati ya kiasi hicho, Sh trilioni 13.35 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh trilioni 4.052 kwa matumizi ya maendeleo. Akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya serikali kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango (pichani) alisema:“Mfumo na ukomo wa bajeti umezingatia hali halisi ya upatikanaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali.”

Mapato ya ndani Dk Mpango alisema mapato ya ndani, ikijumuisha mapato ya halmashauri, yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 20. 895 sawa na asilimia 64 ya bajeti yote. Kati ya mapato yote, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh trilioni 18.0 sawa na asilimia 13.6 ya Pato la Taifa, huku mapato yasiyo ya kodi yanatarajia kufikia Sh trilioni 2.158 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni Sh bilioni 735.6.

Vyanzo vingine vya mapato Dk Mpango alisema vyanzo vingine vya mapato ni pamoja na misaada na mikopo yenye masharti nafuu ya Sh trilioni 2.676 kutoka kwa washirika wa maendeleo, ikiwa ni asilimia 8 ya bajeti yote. Alisema serikali pia inatarajia kukopa Sh trilioni 5.793 kutoka soko la ndani, ambapo Sh trilioni 4.6 kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zilizoiva na Sh trilioni 1.19 ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Alisema Sh trilioni 1.19 ambazo ni mikopo mipya ni sawa na asilimia 0.9 ya Pato la Taifa.

“ Ili kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi muhimu ya miundombinu, serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 3.1,” alisema. Matumizi kwa mwaka 2018/19 Waziri Mpango alisema serikali imepanga kutumia Sh trilioni 32.476, kati ya fedha hizo Sh trilioni 20.47 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya bajeti. “Matumizi ya kawaida yanajumuisha Sh trilioni 10 kulipia deni la serikali, Sh trilioni 7.37 mishahara, Sh trilioni 3.09 matumizi mengineyo na Sh bilioni 389.9 matumizi yatokanayo na vyanzo vya ndani vya halmashauri,” alisema.

Matumizi ya maendeleo Dk Mpango alisema serikali itatumia Sh trilioni 12 sawa na asilimia 37 ya bajeti, kiasi kinachojumuisha Sh trilioni 9.876 sawa na asilimia 82.3 ni fedha za ndani na Sh trilioni 2.130 sawa na asilimia 17.7 ni fedha za nje. “Kiasi hiki hakihusishi uwekezaji wa moja kwa moja wa sekta binafsi, mashirika ya umma na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi. Pia serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kuwezesha mashirika ya umma na sekta binafsi kutekeleza miradi ya maendeleo.” Aliongeza: “Bajeti inalenga katika kuendelea kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha ustawi wa jamii.

Serikali itaendelea kujizatiti katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuendelea kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi. “Kwa upande wa matumizi, serikali itaendelea kuweka mkazo katika usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ili zitumike zaidi kugharamia miradi ya kipaumbele na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.” Vipaumbele mwaka 2018/19 Waziri Mpango alisema miradi itakayopewa msukumo wa kipekee ni mradi wa kituo cha kuzalisha umeme wa maji katika Mto Rufiji (MW 2100), ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge hususani vipande vya Dar es Salaam hadi Morogoro (Km 300), na Morogoro hadi Makutupora (km 336).

Pia uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania, ujenzi wa bomba la kusafirishia mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, uzalishaji wa makaa ya mawe na umeme-Mchuchuma-Liganga, uendeshaji wa shamba la miwa na ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi. Pia mradi wa Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini, uendeshaji wa Kiwanda cha Kusindika Gesi Asilia kuwa kimiminika-Lindi na kuongeza idadi ya wataalamu katika fani adimu.

Mradi kukuza uchumi wa viwanda Dk Mpango alisema serikali inalenga kuendelea kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wiki nchini, hususani za kilimo, madini na gesi asili. Katika eneo hili, miradi itakayopewa kipaumbele ni kuimarisha shughuli za Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), Kiwanda cha Ngozi na Bidhaa za Ngozi-Karanga, Mradi wa magadi Soda- Bonde la Engaruka, Kituo cha zana za Kilimo na Ufundi Vijijini-CARMATEC na viwanda vya Nyumbu na Mzinga.

Miradi ya maendeleo ya viwanda, watu Dk Mpango alisema serikali imelenga kuendeleza mafanikio ya upatikanaji wa huduma za msingi kwa ustawi wa maisha ya Watanzania, kwa kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa maktaba za mikoa na ujenzi na uboreshaji wa maabara katika shule na taasisi. Ipo pia miradi ya kuendeleza ujenzi na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji, kupanua huduma za elimu ya afya na usafi wa mazingira shuleni, mijini na vijijini na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma kwa ngazi zote, ikiwamo zahanati, vituo vya afya, hospitali za mikoa, kanda na kitaifa.

Miradi mingine ni kukamilisha ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi vya wilaya na mikoa, utoaji wa mikopo wa wanafunzi wa elimu ya juu na kuimarisha programu za kukuza ujuzi. Mpango alisema serikali imepanga kutekeleza ujenzi na ukarabati wa mundombinu, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa Reli ya Kati na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ikiwa ni pamoja na ununuzi wa injini na mabehewa, ujenzi wa barabara zinazounganisha makao makuu na mikoa na masoko ya kikanda na barabara za kupunguza msongamano na miradi ya kuzalisha na kusambaza umeme.

Mpango alisema serikali imelenga pia kuimarisha mifumo ya kitaasisi, kwa lengo la kuimarisha ufuatiliaji na tathimini kwa kuzingatia mwongozo wa usimamizi wa uwekezaji wa umma na kuimarisha mifumo ya kuhifadhi na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi kulingana na thamani ya fedha.

Mikakati ya sekta za kilimo Kwa mujibu wa Dk Mpango, katika kuchochea ukuaji wa sekta za kilimo, serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, kuongeza upatikanaji wa zana na pembejeo za kilimo, kuongeza huduma za ugani, kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya hifadhi ya mazao na masoko na kutatua vikwazo mbalimbali vinavyosababisha viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi zitokanazo na kilimo kushindwa kushindana na bidhaa husika kutoka nje.

Alisema mpango unasisitiza ujenzi wa mazingira yatakayochochea na kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Pamoja na hatua za kuondoa vikwazo katika uwekezaji na ufanyaji biashara. “Mpango umezingatia utekelezaji wa mapendekezo ya marekebisho ya sheria, kanuni na taratibu kwa miradi ya ubia na kuhakikisha upatikanaji rahisi wa maeneo ya uwekezaji, kuandaa Sera ya Maendeleo ya Sekta Binafsi, kuimarisha mfumo rekebu na miundo – taasisi na kuimarisha mfumo wa majadiliano kati ya serikali na sekta binafsi.”

Dk Mpango alisema serikali inategemea kufanya upembuzi yakinifu kuainisha uwezekano wa kutekeleza miradi kwa utaratibu wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi ambayo ni miradi ya bandari ya Mwambani, reli ya Mtwara-Mchuchuma/ Liganga kwa kiwango cha Standard Gauge, reli ya Tanga-Arusha-Musoma kwa kiwango cha Standard Gauge, ujenzi wa miundombinu ya reli na uendeshaji wa treni ya abiria katika jiji la Dar es Salaam, usambazaji wa gesi asilia nchini na mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Awamu ya II hadi IV.

Mwenendo wa mapato, matumizi mwaka 2017/18 Mpango alisema hadi Januari, mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia Sh trilioni 17.4 sawa na asilimia 85 ya lengo la kipindi cha mwaka 2017/18 ambapo mapato ya kodi yalikuwa Sh trilioni 10 sawa na asilimia 88.3 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 11.36 huku mapato yasiyo ya kodi yalikuwa Sh trilioni 1.456 sawa na asilimia 98.2 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 1.48. Alisema mapato yaliyokusanywa na halmashauri yalikuwa Sh bilioni 345.9 sawa na asilimia 74.1 ya makadirio ya Sh bilioni 466.9 huku misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilifikia Sh trilioni 1.41 sawa na asilimia 66 ya lengo la Sh trilioni 2.15.

Mikopo ya ndani ilifikia Sh trilioni 3.931 ikiwa ni asilimia 95.6 ya kiasi kilichopangwa kukopwa, ikijumuisha Sh trilioni 3.25 zilizokopwa kulipia amana za serikali zilizoiva na mikopo mipya ya Sh bilioni 685.0 na mikopo ya nje ya kibiashara ilifikia Sh bilioni 224.1.

Mpango alisema katika maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mgawo wa bajeti ni kulipa deni la serikali na mishahara ya watumishi wa umma, kugharamia ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege, kulipia malimbikizo ya madai ya wazabuni, wakandarasi na watumishi wa umma, kuendelea na utekelezaji wa miradi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme na kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; kugharamia elimu-msingi bila ada, utekelezaji wa miradi ya maji; na kununua dawa na vifaa tiba.

The post Ni bajeti ya kupaa kimaendeleo appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini