Waombaji ajira mpya wateswa na vyeti

BAADA ya kuwapo kwa waombaji wa ajira katika utumishi wa umma kubainika kutumia vyeti vya kughushi, mamia pia wamebainika kutoa taarifa za kupotolewa kwa vyeti vyao vikiwamo vya Kidato cha Nne.


Tangu Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilipoanza kutolewa vibali vya ajira mwaka 2010 hadi 2015/2016, ilizuia waombaji kazi 1,951 waliotaka kutumia vyeti na nyaraka za kughushi ili kujipatia fursa ya kuajiriwa katika utumishi wa umma bila ya kuwa na sifa stahili. Aidha, Sekretarieti ya Ajira tangu kuanza kutolewa kwa vibali vya ajira baada ya kusitishwa kwa mwaka 2016/17, imefanikiwa kuzuia waombaji kazi waliowasilisha maombi yao ya kazi kupitia Sekretarieti ya Ajira zaidi ya 45.
Serikali ya Awamu ya Tano ilifanya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma vya Kidato cha Nne na kubainika kuwa watumishi zaidi ya 16,000 wanatumia vyeti vya kughushi. Februari mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliwaambia waandishi wa habari kuwa serikali imeokoa Sh bilioni 84.22 sawa na asilimia 66 ya malimbikizo ya awamu baada ya kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara watumishi hewa, wenye vyeti feki na wasio na sifa.
Hata hivyo, licha ya kuondolewa kwa watumishi hao wenye vyeti feki, imebainika kuwa waombaji 893 wa ajira katika utumishi wa umma, wametoa taarifa za upotevu wa vyeti kutoka Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA). Haijafahamika wazi kwa nini kumekuwapo na idadi kubwa ya waombaji hao walipoteza vyeti vyao, lakini kuwapo kwa taarifa hizo kunahusishwa na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kuhakiki vyeti vya watumishi wake.
Takwimu za mchakato wa ajira katika Sekretarieti ya Ajira zinaonesha kuwa tangu serikali ilipofungua ajira wamepokea kutoka mamlaka za ajira vibali vya ajira 306. Kwa mujibu wa taarifa ya sekretarieti hiyo, imeshatangaza nafasi wazi za kazi zipatazo 2,828, imepokea jumla ya maombi 76,462, na kufikia mwezi uliopita, imeshawapangia vituo vya kazi waombaji waliofaulu usaili wapatao 2,223. Kati yao, nafasi za watendaji wakuu wa taasisi za umma ni 12. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nafasi ambazo mchakato wake upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni 605.
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilianzishwa Machi, 2009 kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya Mwaka 2002. Ni chombo maalumu huru cha kushughulikia mchakato wa masuala ya ajira katika utumishi wa umma kwa niaba ya Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi mbalimbali za umma. Ilianza kutekeleza majukumu yake Juni, 2010.
Moja ya mafanikio ya Sekretarieti ya Ajira ni kuisaidia serikali kupunguza tatizo la ukosefu wa watumishi wa kutosha kwa baadhi ya maeneo ambayo awali yalionekana kukosa wataalamu hasa maeneo ya pembezoni. Suala hili linaenda sambamba na kuajiri watumishi wenye sifa na kupunguza tatizo la ukabila, rushwa na upendeleo kwa kuhakikisha mchakato wa ajira unazingatia misingi ya haki, usawa na uwazi kwa kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Hata hivyo, Sekretarieti ya Ajira imeeleza kuwa kumekuwapo na changamoto za jumla ikiwamo baadhi ya wadau kuwa na fikra hasi.
“Tunaendelea kuelimisha umma kuhusu Sekretarieti ya Ajira inavyofanya kazi pamoja na kuhakikisha tunatoa huduma kwa wakati, viwango, uwazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu,” ilieleza. Changamoto nyingine ni baadhi ya waombaji wa kazi kughushi sifa za kielimu, taarifa binafsi, nyaraka na pia sifa za kitaaluma. Aidha, ipo changamoto ya baadhi ya wahitimu kuwa na uwezo mdogo; asilimia kubwa ya wasailiwa kuwa na uwezo mdogo wa kujieleza kwa lugha rasmi za usaili ambazo ni Kiswahili na Kiingereza na hivyo kushindwa kuwasilisha vizuri majibu ya usaili kwa kile alichofundishwa chuoni na hivyo kupelekea Sekretarieti ya Ajira wakati mwingine kushindwa kujaza baadhi ya nafasi na kurudia upya mchakato mzima.

Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini