Waziri Shonza: Nimesikia Malalamiko ya Daimond Mimi Siwezi Kujibizana Naye

Nimesikia Malalamiko ya Daimond Mimi Siwezi Kujibizana Naye
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, amesema amesikia malalamiko ya mwanamuziki Diamond lakini hawezi kumjibu kwa sababu zipo taratibu za kufuata kama anaona hajatendewa haki.

Shonza analijibu hilo ikiwa ni siku moja tangu mwanamuziki  'Diamond' amtaje waziri huyo katika malalamiko yake, akidai amekuwa akikurupuka  na kutolea mfano wa kufungia nyimbo na wasanii wakati akihojiwa na kituo cha redio cha Times.

Waziri huyo amesema hayupo tayari kumjibu Diamond  ingawa wasanii wanapaswa kuelewa kuwa hakuna aliye juu ya sheria hata kama msanii mkubwa namna gani.

"Aliyewafungia wasanii si Shonza bali ni mamlaka na kama mlivyoona safari hii hadi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeingilia kati suala hilo, sasa mtu anaporusha tuhuma kumlaumu Shonza atakuwa hanitendei haki. Isitoshe ofisi zetu zipo wazi anayeona ameonewa afuate taratibu katika kudai haki yake na si kulalamikia pembeni," amesema Waziri Shonza.

Kuhusu kutoitwa kwa wasanii kabla ya kufungiwa kwa nyimbo zao Shonza amesema hilo waulizwe Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) maana ndio wenye kujua sababu na kwa baadhi ambao aliwaita ameeleza kuwa ni kutokana na kupewa maagizo ya kubadilisha nyimbo zao na kuwahi kukiri makosa lakini wakashindwa kutekeleza.

Katika mahojiano hayo na redio Times, Diamond alielekeza mashambulizi zaidi kwa Waziri Shonza na kudai kwamba amekuwa akifanya maamuzi yake kwa kukurupuka akisahau kwamba viongozi hawana mchango wowote kwao na pia wamekuwa wakiziumiza familia zao.

"Hivi leo unanifungia nyimbo yangu niliyoitengeneza kwa mamilioni ya pesa unadhani nitazirudishaje, au unadhani watoto wangu Nillan, Dyllan na Tiffah watanunuliwa na nini ‘pampas’? Ifike mahali viongozi wetu wavae viatu vyetu na si kuona raha tu kutufungia wakati tumetaabika katika kuyajenga majina yetu hadi sasa tunajulikana duniani," amesema Diamond.

Februari 28 TCRA iliandika barua kwa vituo vya redio na televisheni ikiviagiza visitishe kuonyesha nyimbo 15 za wasanii kadhaa kutokana na kuwa na maudhui ambayo yanaenda kinyume na maadili na kanuni za Huduma za Utangazaji(Maudhui) 2005.

Nyimbo hizo na jina la msanii aliyeimba  kwenye mabano ni  Hallelujah na Wakawaka (Diamond), Kibamia (Roma Mkatoliki), Pale Kati patamu, Maku (Makuzi) na Mikono Juu (Ney wa Mitego), Hainaga Ushemeji(Manifongo), I am Sorry JK(Nikki Mbishi.

Nyingine ni Chura (Snura) na Nimevurugwa (Snura), Tema mate tumchape(Madee), Uzuri wako(Jux), Nampa papa(Gigy Money), Nampaga(Baranaba) na Bongo Bahati mbaya(Young D).


Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini