Zitto adai kubanwa kila kona

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amedai anaendelea kubanwa kila kona baada ya kuzuiwa mikutano yake kadhaa, huku baadhi ya viongozi na wanachama wa chama hicho wakijiondoa na kujiunga na CCM.

Hadi sasa Zitto anasema mikutano minne imezuiwa katika mikoa mbalimbali ukiwamo wa Manyara, Mwanza na Tabora ambako ile ya Kaliua na Urambo ilizuiwa.

Mikutano hiyo ni sehemu ya ziara yake ya kuimarisha chama hicho sanjari na kukutana na kuzungumza na madiwani wake.

Hata hivyo, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini alisisitiza jana kuwa ataendelea na ziara kama kawaida kwa sababu wanakutana na wananchi ambao wanaeleza kero mbalimbali wanazokumbana nazo katika maeneo wanayoishi.

Juzi Jeshi la polisi wilayani Kaliua lilizuia mkutano wa hadhara wa mbunge huyo kutokana na kile walichodai kuwa wamepata taarifa za kiintelijensia kuwa ACT wanataka kufanya maandamano makubwa ambayo yatasababisha uvunjifu wa amani.

Taarifa hiyo ya polisi kwenda kwa Zitto iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ilieleza kuwa inazuia mikutano hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Wasaidizi ya mwaka 1985 (Cap 322) iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002 katika kifungu cha43 (3) na cha 44 cha sheria hiyo. Barua hiyo ilisainiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kaliua (SSP), Lucas Mgaya.

Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Tabora Wilbroad Mutafungwa kueleza kwa undani kuhusu taarifa hiyo, ambaye alisema hawezi kuzungumza kwa kuwa hayupo katika nafasi nzuri.

“Nipo kanisani naomba unitafute kesho nitakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia jambo hilo,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Pamoja na mikutano yake kuzuiwa, kadhalika chama chake kimepata mapigo kadhaa ya kuondokewa na wanachama na viongozi wake, ikiwamo Machi 2 ambapo watu 12 waliodai ni viongozi walitangaza kukihama.

Katibu wa Itikadi na Mawasiliano, Ado Shaibu alisema baadhi ya waliohama si viongozi na wengine walivuliwa madaraka muda mrefu.

Juzi, Diwani wa chama hicho, Kata ya Gehandu wilayani Hanang, Mathayo Samhanda alitangaza kujiuzulu nafasi yake na kukihama.

The post Zitto adai kubanwa kila kona appeared first on Mtembezi.


Sponsored by SOMA ZAIDI

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini