Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtaka Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole kuwa makini na kauli zake anazozitoa kuhusu mikutano ya hadhara lasivyo itakuja kumtokea kama Mwigulu Nchemba alivyofanyiwa.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema baada ya kupita siku kadhaa tokea Polepole alivyotoa kauli yake kuwa 'mikutano ya hadhara haijapigwa marufuku ila imewekewa utaratibu mzuri zaidi wa namna ambavyo wanapaswa kufanya siasa katika nchi huku akidai tatizo kubwa sio mikutano hiyo kutofanyika bali ni viongozi wa upinzani kuishi nje ya majimbo yao'.
"Hicho anachokifanya Polepole ni propaganda nyepesi tu na nimshauri kwamba kwa sasa ajifunze kupitia Mwigulu Nchemba maana naye alikuwa anasema hivyo hivyo kuwa mikutano haijazuiliwa lakini yeye mwenyewe ni juzi tu wamemzuia kufanya mikutano jimboni kwake kabla ya kumruhusu.
"Anavyosema mikutano haijazuiliwa yeye ndio anakuwa kinara sasa wa kupotosha umma juu ya suala hilo na wala sio sisi", amesema Mrema.
Pamoja na hayo, Mrema ameendelea kwa kusema "hoja yake ambayo anasema Wabunge wetu hawaishi katika majimbo yao ni dhaifu na mufilisi kwasababu Wabunge wetu ndio wanaongoza kukaa katika maeneo yao kuliko wowote wale na pia Wabunge wetu wamezuiliwa kufanya mikutano yao katika baadhi ya maeneo na tuna barua rasmi ya kuzuiliwa".
Sponsored by
ZAMOTO MEDIA
0 Comments