Hii Ndio Idadi ya Wachezaji Anayoitaka Kocha wa Simba

Hii Ndio Idadi ya Wachezaji Anayoitaka Kocha wa Simba
Kocha Mkuu wa Simba, Mrundi, Masoud Djuma, amesema kuwa kikosi chake kinahitaji kuwa na wachezaji 27 pekee huku akiahidi kuwatoa kwa mkopo baadhi ya wachezaji wasiokuwa na kiwango katika timu huku jina la kipa Emmanuel Mseja likiwa la kwanza.

Kauli hiyo, aliitoa juzi jioni baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Beach Veterani jijini Dar es Salaam.

Simba tayari imefanikiwa kuwasajili wachezaji sita hadi sasa ambao ni Adam Salamba, Mohammed Rashid, Meddie Kagere, Abdul Mohammed, Marcel Boniventure na Pascal Wawa.

Akizungumza na Championi Jumatano, Djuma alisema katika usajili huo wa wachezaji 30, wanataka kubakisha nafasi tatu pekee kwa ajili ya kuongeza katika usajili wa dirisha dogo kama akihitajika mchezaji kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chao.

Djuma alisema, wachezaji watakaobaki kuichezea Simba ni wale watakaoweza kupambana ndani ya uwanja katika kuipa matokeo mazuri huku akiahidi kuwaondoa baadhi ya wachezaji wenye mikataba kwenda kwenye klabu nyingine kwa ajili ya kulinda viwango vyao.

“Sidhani kama ni sawa kuendelea kukaa na mchezaji mwenye mkataba kwenye timu wakati hana nafasi ya kucheza katika kikosi changu, hivyo nimeona ni vema nikamuachia kwenda kwa mkopo kwingine kwa ajili ya kwenda kucheza kuliko aendelee kukaa benchi.

“Hivyo, hiyo inaweza kumsababishia mchezaji kuua kiwango chake kama mfano kipa wetu Mseja msimu uliopita wa ligi hakupata nafasi ya kucheza, hivyo kama kocha nimeshauri tumtoe kwa mkopo ili aende kwingine akacheze.

“Na hilo tayari nimelifanyia kazi na kuutarifu uongozi, hivyo Mseja hatakuwa katika sehemu ya kikosi chetu, pia wapo wengine ambao hivi karibuni nitawaweka wazi,” alisema Djuma.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini