Mwakyembe awachamba wasanii


Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, amesema kanuni wanazolalamikia wasanii za tozo mbalimbali hazikuja kwa bahati mbaya.


Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe,

Dkt. Mwakyembe ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam, wakati akizungumza na wanahabari pamoja na wasanii  baada ya kuwepo na malalamiko ya wasanii tangu Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lilipotangaza kanuni mpya zinazotaka waandaaji wa maonyesho ya wanamuziki, kulipa kuanzia Sh50,000 hadi Sh5 milioni.

Dk Mwakyembe amesema vikao mbalimbali vilikaa na kupitisha kanuni hizo na kwamba wasanii wanaolalamikia suala hilo ni wale ambao hawakuhudhuria kwenye vikao hivyo.

Katika kikao hicho Waziri Mwakyembe amewalaumu wasanii wengi wenye majina makubwa kutohudhuria vikao, ambapo kati ya vikao walivyowahi kukaa ndivyo vilivyopitisha sheria ambazo zilianza kutekelezwa tangu Julai Mosi mwaka huu.

"Wasanii hamuhudhurii vikao, mnasubiri kuja kulalamika sheria na kanuni zikishapitishwa, kwani wengi mkishapata majina mnapandisha mabega juu na kujiona nyie ndio nyie hata mkiitwa katika mambo yenye faida kwenu hamji,”amesema.

"Nina uhakika hakuna kampuni kubwa zinashindwa kulipa Sh5 milioni, nashangaa nyie mnavyowatetea wakati wao hata mmoja mpaka sasa hivi hakuna aliyenijia kulalamika," amesema Mwakyembe.

Pamoja na hayo Mwakyembe amewapa rungu wasanii kung'oa mabango ya matangazo yenye picha zao endapo mkataba na kampuni husika utakuwa umekwisha.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini