Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema ana matumaini makubwa na timu ya taifa ya soka la wanawake Tanzania, Twiga Stars kurejea na ubingwa wa CECAFA Challenge Cup.
Wallace Karia amesema kuwa licha ya changamoto ndogo ndogo zilizotokea katika maandalizi ya mashindano hayo, anaamini kuwa vijana wake wamejipanga vizuri zaidi mwaka huu kuhakikisha wanatetea ubingwa huo.
"Tunatarajia timu itaingia kambini mjini Bukoba Julai 10 mwaka huu na itafanya mazoezi na kuondokea pale kuelekea Kigali, Rwanda tayari kwa mashindano hayo. Tunajua mashindano yatakuwa magumu sababu tumeongea na wenzetu na wamejipanga lakini sisi kama mabingwa watetezi tunasema tutarudi na kombe".
Rais wa TFF pia amesema waandaaji wa mashindano hayo, nchi ya Rwanda walikuwa wakitoa sababu za msingi zilizopelekea kuahirishwa kwa mashindano hayo mara kwa mara ingawa ilileta changamoto katika matayarisho ya timu.
Naye kocha wa timu hiyo ya Twiga Stars, Edna Lema amesema kuwa wachezaji wake wana morali kubwa ya mashindano licha ya kuahirishwa wakati wakiwa kambini.
"Kwanza sisi kama timu tumefurahi kusikia taarifa hiyo kwasababu kuna kipindi ambacho tuliingia kambini karibia mwezi mzima tukaambiwa mashindano yameahirishwa. Lakini kikubwa tumejiandaa kisaikolojia kuhakikisha tunafanya vizuri kama bingwa mtetezi".
Twiga Stars ilishinda ubingwa huo mwaka uliopita nchini Uganda na sasa wanakwenda kutafuta historia mpya ya kutetea ubingwa wao.
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments