Watiwa mbaroni kwa tuhuma za kuua na kuchoma moto


WATU wawili wakazi wa kata ya Ruiwa wilayani Mbarali wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mkulima Shukrani Ismail (29) na kisha kuuchoma moto mwili wake. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amewataja watuhumiwa wanaowashikilia kuwa ni Shabani Ramadhani (19) na Salum Ramadhani (39) wote wakazi wa Ruiwa wilayani Mbarali. 

Akizungumzia tukio hilo, Matei alisema Julai 9, mwaka huu, Ismail aliondoka nyumbani kwake ambapo hakuonekana tena hadi maiti yake ilipopatikana Julai 12, ikiwa imechomwa moto katika mashamba ya mpunga. 

Amesema kabla ya kukumbwa na mauti kulikuwa na mgogoro wa mashamba baina ya Ismail na watuhumiwa na kwamba polisi wanaendelea na upelelezi. 

Wakati huo huo, waganga watatu wanaodaiwa kuwa wa jadi wapiga ramli, wakiwemo wawili kutoka mkoani Tabora wanashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na nyara ya serikali. 

Kamanda Matei amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Peter Daudi (34), mkazi wa mlima Njiwa wilayani Chunya, wengine ni Seif Juma na Salum Moses wote wakazi wa Tabora. 

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na pembe ya tandala kinyume cha sheria na kwamba uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Sponsored by ZAMOTO MEDIA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini