Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimewataka wanachama wake nchi nzima kufika mahakamani wakati kesi inayowakabili viongozi wake watano itakapounguruma ili wajionee uendeshwaji wa kesi na kuamua kwa pamaoja nini cha kufanya.
Wito huo wa CHADEMA umekuja saa chache baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kuamua kufuta dhamana ya viongozi wawili wa chama hicho, Mwenyekiti wa chama taifa, Freeman Mbowe na Mbunge wa Jimbo la Tarime mjini, Ester Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.
Akizungumza na wanahabari, makao makuu ya chama hicho yaliyopo mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Vicent Mashinji amesema, "wanachama wa CHADEMA nchi nzima, suala hili ni zito, ni nyeti na linahusu mustakabali wa nchi yetu, usisubiri kusimuliwa njoo uone mwenyewe kinachoendelea mahakamani kwasababu kumekuwa na upotoshaji mkubwa".
"Tunaomba tuje tusikilize wenyewe mahakamani na baada ya hapo tuamue ni hatua gani tutachukua sisi kama watetea haki wa watu wote katika taifa hili," ameongeza.
Aidha katika hatua nyingine, chama hicho kimeazimia kukata rufaa katika Mahakama Kuu kwa kile ilichokidai ni kupinga juu ya hatua ya kufuta dhamana ya viongozi wake iliyofanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi.
"Tumeamua kukata rufaa kwenda Mahakama Kuu na tumeshawasilisha barua yetu, bado tunasubiria watupe namna. Na katika barua yetu tumeeleza haya mashaka yetu yote juu ya mwenendo wa hii kesi".
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments