MPENZI msomaji wangu, kasi ya kusalitiana kwa wapenzi imekuwa ikiongezeka kila kukicha kiasi kwamba unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi unahisi kama unaingia kwenye matatizo makubwa na hii ni kwa sababu watu siyo waaminifu kabisa kwa wapenzi wao. Unaweza kuwa na mpenzi wako ambaye kila mnapoonana anakueleza kuwa, hawezi kukusaliti na atakuwa na wewe katika shida na raha.
Lakini huyohuyo usishangae siku moja ukamkuta yuko na mtu mwingine. Swali la kujiuliza ni kwamba, kwa nini wapenzi wanachepuka? Hicho ndicho nilichopanga kukizungumzia leo. Yaani nitaainisha baadhi ya mambo ambayo kwa uchunguzi wangu nimebaini ndiyo yanayochangia walio wengi kuchepuka, wawe wako kwenye ndoa au uhusiano wa kawaida.
TAMAA ZA KIMWILI NA PESA
Tamaa hasa ya pesa imekuwa ikiwashawishi watu kushindwa kujizuia kuwasaliti wapenzi wao. Kwa wale ambao wako kwenye ndoa wakati mwingine hasa wanawake wasipopatiwa mahitaji yao muhimu na akatokea jamaa na kumhakikishia kwamba atampatia kila anachotaka, wanakubali mara moja bila kujua kwamba wao ni wake za watu ama wapenzi wa watu na kujikuta wanajenga mazoea. Wengine wanapatiwa kila kitu na waume zao lakini sasa kinachotokea ni tamaa za kimwili tu ambazo zinawasumbua na kujikuta wanatafuta wanaume wengine huku wakidai kuwa wanatafuta ladha tofauti. Hili si kwa wanawake tu hata wanaume pia, unaweza kumkuta ana mwanamke bomba tu mwenye kila kigezo, lakini bado anakuwa na tamaa za kutafuta kimwana mwingine nje.
TABIA ZISIZORIDHISHA
Wapo ambao wanaishi maisha ya ajabu sana, yaani wanaishi katika ndoa ama ndani ya uhusiano wakielekea kwenye kuoana lakini hawaaminiani kabisa, kila mtu anakuwa na wasiwasi juu ya mwenzake. Afadhali sasa iwe kutokuaminiana tu lakini wapenzi wanakuwa hawasalitiani. Kuna wale ambao ni wazi hawatulii katika mahusiano yao, yaani matendo yao tu yanaonesha dhahiri kwamba, uaminifu ni sifuri. Kuwa karibu sana na watu wa jinsia tofauti na kuwa na mawasiliano nao ya siri au mwanamke anapomuwekea mumewe vikwazo katika tendo la ndoa anatarajia akafanye na nani kama siyo kumwambia akatafute wengine nje? Ndiyo maana wanaowanyima unyumba waume zao hata wanaposikia kwamba wanasalitiwa wanakuwa hawana nguvu ya kuwashutumu wapenzi wao, utamshutumuje wakati wewe humtimizii katika mambo flani? Si hivyo tu, kwa wanaume nao wengine wamekuwa wakiwasusa wake zao na kukaa siku mbili ama zaidi bila kuonekana nyumbani ama kama atarudi basi usiku wa manane akiwa amelewa na hana mpango kabisa na mke wake. Katika mazingira hayo unadhani nini kinaweza kutokea kama siyo mwanamke kutafuta mwanaume atakayempatia mapenzi?
KUWEPO KWA MAPENZI YA KILAGHAI
Tunapozungumzia mapenzi tunaweza kuyagawanya katika makundi mawili, mapenzi ya kweli na mapenzi ya uongo. Walio katika mapenzi ya kweli huwezi kuwasikia wamesalitiana. Ila wale walio katika mapenzi ya kudanganyana kusalitiana ni kitu cha kawaida kwao hivyo kujikuta kila siku wakifumaniana.
UDHAIFU KWA WAPENZI
Udhaifu ambao umezungumziwa hapa ni wa kimaumbile ambao hata hivyo wataalam wa masuala ya mapenzi wanaeleza kwamba, haiwezi kuchukuliwa kama sababu ya kumsaliti mpenzi wako uliyempenda kwa dhati. Kwa mfano, mwanaume unakuwa ‘Functionless’ yaani jogoo hawiki (tatizo ambalo si la kujitakia) na mke wake hayuko tayari kuendelea kuwa naye hivyo kulazimika kuomba talaka. Lakini mwanaume anakuwa mgumu wa kutoa talaka kutokana na jinsi anavyompenda.
Wengi wao wanachokifanya ni kuendelea kuwa katika ndoa huku wakiangalia uwezekano wa kuwa na uhusiano na mtu mwingine wa nje. Kwa wanawake nao yawezekana mwanamke hazai (tatizo ambalo si la kujitakia pia) na mwanaume anahitaji mtoto, atakachokifanya ni kutoka nje kwa siri lakini pia inaweza kufikia hatua mwanamke akagundua. Kwa kifupi ni kwamba kusalitiana kwa wanandoa kumekuwa kukitokea kutokana na kuwepo kwa mazingira fulani ambayo baadhi yao wamekuwa wakishindwa kujizuia nayo na hivyo kujikuta wanatoka nje ya mahusiano.
Ila sasa nalazimika kwa nguvu zote kuwashauri wale walio katika uhusiano wa kimapenzi, namaanisha wapenzi wa kawaida, wachumba ama wanandoa, tusiwe na tamaa za kijinga na kufikia hatua ya kuwasaliti wapenzi wetu. Hivi unajisikiaje unapomvulia nguo mtu ambaye wala hana ‘future’ na wewe? Hivi na wewe ukifanyiwa hivyo na mpenzi wako utajisikiaje? Elewa maumivu utakayoyapata pale utakaposikia mpenzi wako ana uhusiano na fulani ni hayohayo atakayoyasikia mwenza wako. Kuwa muaminifu, ridhika na unachokipata kwake, muoneshe mapenzi ya dhati naye atafanya hivyohivyo na kujikuta mnayafurahia maisha yenu.
Sponsored by
ZAMOTO MEDIA
0 Comments