Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema askari wote walioshiriki katika mapambano na kuwaua watu wanaosadikika kuwa majambazi saba Novemba 15, 2018 jijini Mwanza watapandishwa vyeo.
Tukio hilo lililotumia takribani dakika 45 lilitokea katika Kata ya Kishili jijini hapa saa tano usiku.
Akizungumza na maofisa wa polisi na baadhi ya askari wa vikosi vyote vya polisi jijini hapa leo Ijumaa Novemba 23,2018 katika viwanja vya polisi Mabatini, Waziri Lugola amesema hiyo ndiyo njia pekee ya kuwapongeza askari hao.
"Askari hawa wamefanya jambo la kizalendo kupambana na majambazi hao wanaosumbua raia wetu, kwa hiyo inapotokea askari wanatutoa kimasomaso lazima tuna kila sababu ya kuwafanyia jambo la kuwafurahisha, hivyo na hawa tunawapandisha vyeo wote," amesema Lugola.
Hata hivyo, amesema bado majambazi wapo na ni wajibu wa askari kuhakikisha wananchi na mali zao wanakuwa salama kwa kupambana nao.
"Ni kosa kwa askari kuwa mwoga hupaswi kukimbia tukio, lazima ukabiliane nalo maana ndio dhamana tuliyokabidhiwa," amesema.
Ligola ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi wapo salama na kuwatumia salamu wanaofanya uhalifu kwamba bora wajisalimishe na kuacha mara moja vitendo hivyo vinginevyo watashughulikiwa popote watakapokuwa hata kama ni mapangoni maana Serikali ina mkono mrefu.
Awali, Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana amesema mkoa huo upo shwari licha ya kuwapo matukio kadhaa ya wahalifu lakini wamekuwa wakiwadhibiti kabla ya kutekeleza azma yao.
"Mkoa upo shwari, vikosi vyetu vimejipanga kuwashughulikia wanaoleta ujuaji kufanya uhalifu kwenye mkoa wetu, nikuhakikishie tupo vizuri,” amesema
Sponsored by ZAMOTO MEDIA
0 Comments