Jeshi la Polisi Jijini Dodoma linaendelea na misako katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo ambapo limefanikiwa kukamata watuhumiwa 64 wakiwemo Wezi, Makahaba na Wauza Madawa ya kulevya.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu kukamatwa kwa watuhumiwa 64 kati yao wakiwamo 11 wa ukahaba, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gilles Muroto, alisema kuwa jeshi hilo litaendelea kuwakamata watu hao kwa kuwa wanachafua taswira ya jiji hilo.
Kamata kamata ya watu wanaofanya biashara hiyo, ilianza Oktoba 9, mwaka huu na kukamata makahaba 22, wanaume watano waliokuwa wakiwanunua pamoja na wamiliki wanne wa maeneo yanayoruhusu biashara hizo.
Aidha, Oktoba 31, mwaka huu, jeshi hilo liliwakamata watu wengine 17 wanaotuhumiwa kufanya biashara hiyo.
"Watuhumiwa hawa wote watafikishwa mahakamani na jeshi letu litaendelea na msako wa kuwakamata makahaba wote jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa ndiye balozi wetu wa kupinga maambukizi mapya ya Ukimwi,hivyo hatuwezi kuendelea kuwavumilia hawa watu," alisema Muroto.
Alisema kumekuwa na ongezeko la biashara hiyo kwa kasi, hivyo ni vyema watu wakachukua tahadhari kujiepusha na ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo.
Alisema kuwa watuhumiwa hao wote wamekamatwa katika msako uliofanywa na jeshi hilo katika maeneo mbalimbali.
Alisema kuwa msako huo ulihusisha pia ukamataji wa mali za wizi na wapokea mali hizo pamoja na wavunjaji wa nyumba za watu na kuiba.
Katika tukio jingine, Muroto alisema wamekamatwa watuhumiwa sita na dawa za kulevya aina ya bangi misokoto 420 ya majani ya bangi, pamoja na kilo tatu za majani ya bangi kinyume cha sheria.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Christopher Edward (25), mkazi wa Chang'ombe, Hafidhu Mohamed (32), mkazi wa Ntyuka na Cosmas Ndalu, mkazi wa Maili Mbili.
Pia walikamatwa watuhumiwa wengine watatu Asha Omary, mkazi wa Chamwino, Tatu Shabani na Ashirafu Hassan, wakazi wa Chang'ombe wakiwa na pombe haramu ya gongo.
Muroto aliongeza kuwa jeshi hilo limemkamata Mkazi wa Chamwino Msafiri Stephano (32) akiwa na mafuta aina ya dizeli lita 100 zinazodaiwa kuwa za wizi.
Katika tukio jingine wamekamatwa watuhumiwa saba kwa makosa ya kuvunja na kuiba wakiwa na mali za wizi mbalimbali
Kadhalika, Muroto aliwataka wananchi wa mkoa huo katika kipindi hiki cha sikukuu kila mtu achukue tahadhali za kuhakikisha usalama katika maeneo yao.
Sponsored by
ZAMOTO MEDIA
0 Comments