BARRICK YASISITIZA KUILIPA TANZANIA BILIONI 682.5

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ( kwa Afrika na Mashariki ya Kati) Bw. Willem Jacobs alipokutana naye kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaa leo Februari 20, 2019 .PICHA NA IKULU

 Kampuni ya Barrick Gold imesema itatekeleza yote yaliyopo katika makubaliano na Serikali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na malipo ya Dola 300milioni sawa na Sh682.5bilioni.


Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Februari 20, 2019 na ofisa mwendeshaji mkuu wa kampuni hiyo anayeshughulikia Afrika Mashariki na Kati, Dk Willem Jacob alipokutaka Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais John Magufuli.


Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa, Jacobs aliyeongozana na washauri wa Barrick Gold Corporation, Rich Haddock, Duncan Bullivant na Wicus du Preez, wamemhakikishia Magufuli kuwa makubaliano yaliyofikiwa Oktoba 19, 2017watayatekeleza kikamilifu.


“Hasa baada ya kampuni kubwa ya uchimbaji dhahabu ya Rand Gold ya Afrika Kusini kuungana na Barrick Gold Corporation katika umiliki, uwekezaji na menejimenti,” inaeleza taarifa hiyo.


Taarifa hiyo inamnukuu Jacobs akibainisha kuwa hakuna kitakachokuwa tofauti na makubaliano yaliyofikiwa awali ambayo yaliongozwa na mwenyekiti mtendaji wa Barrick Gold Corporation Profesa John Thornton.


“Ikiwemo Barrick Gold Corporation kuilipa Serikali ya Tanzania kifuta machozi cha Dola 300 milioni za Marekani (Sh682.5bilioni), kuendelea na uwekezaji kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold na mgawanyo wa mapato ya kiuchumi kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Barrick Gold.


Dk Jacobs amempongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kusimamia maslahi ya Watanzania katika rasilimali za nchi yao na amesema anaunga mkono juhudi zake.


“Mimi ni Mwafrika na sisi sote ni Waafrika, anachokifanya Magufuli ni sahihi kabisa, anahakikisha utajiri wa rasilimali uliopo unabainishwa na unawanufaisha Watanzania, na ndio maana tupo hapa kwa sababu tunakubaliana ,” amesema Jacobs.


“Hivi ndivyo Waafrika tunapaswa kufanya kwa rasilimali zetu, na sisi tunahakikisha tunafanya kazi vizuri na Serikali na jamii kulinda rasilimali hizi, kumbuka rasilimali hizi ni za wananchi, jukumu langu kama mwekezaji ni kubadili hayo madini kuwa kodi na ajira kwa Tanzania na pia kampuni yangu kupata faida yake halali.”



Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini