Bibi Anusurika Kifo Kisa Kuishi Na Wajukuu Wezi....Wananchi Wenye Hasira Kali Wachoma Nyumba Yake

Bibi Anusurika Kifo Kisa Kuishi Na Wajukuu Wezi....Wananchi Wenye Hasira Kali Wachoma Nyumba Yake
Mkazi wa Iringa kata ya Mwangata mtaa wa Ngelewala aliyefahamika kwa majina ya Agusta Sihava amejikuta katika wakati mgumu na kupelekea kuchomewa nyumba yake anayo ishi na wananchi wenye hasira kali wakimshinikiza kuhama eneo hilo kwasababu anaishi na wajukuu wezi.

Ajuza huyo anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka 70 alikumbana na kadhia hiyo ambayo ilimsababishia kupoteza kila kitu na yeye kuponea chupuchupu kuungua na moto baada ya wananchi wenye hasira kali kumtaka ahame eneo hilo vinginevyo atapatwa na mambo mabaya kwasababu ya wajukuu zake.

Aidha wananchi wa mtaa wa Ngelewala walitoa malalamiko yao kuwa wamechoshwa na tabia hizo mbaya kwa maana kila siku wajukuu wa bibi huyo wamekuwa wakiwaibia bila woga wowote .

Mtandao huu umefika mpaka sehemu ya makazi mapya ya bibi huyo ambaye alihamishiwa kwa muda katika nyumba ya Binti yake anayesadikika kuwa ndiye mwenye watoto hao wezi.

Diwani wa kata hiyo ndugu Nguvu Chengula ambaye alijitolea kuezeka na kusakafia nyumba hiyo mpya ya bibi huyo amesema kuwa;

" Huyu bibi anaonewa sana kwa maana hao wajukuu wana wazazi wao ambao ni wazima kabisa lakini wanang'ang'ania kuishi huku ili wawe huru kufanya uhalifu na wazazi wao wanawaangalia  na hawajali kabisa hali hii ambayo kimsingi ni malezi mabovu ya watoto wao"*alisema Nguvu Chengula

Aidha bibi huyo alitolea malalamiko yake kwa watoto wake na wajukuu zake kuwa ndio wanataka kumuua kwasababu ya kufanya uhalifu na kurudi kujificha nyumbani kwake.

"Hawa mabinti zangu hawana shida kabisa ya kuja na kuchukua watoto wao hapa, wameniachia mzigo mkubwa na ukiangalia uwezo wangu kuwatunza ni mgumu kwasababu siwez hata kushika jembe nikalima"alisema bibi Agusta Sihava

Diwani alitoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kuwaachia wajukuu wazee Kwasababu mara nyingi wamekuwa wakishindwa kuwadhibiti wajukuu na hata kuwafanya wawe na uhuru mkubwa wa kufanya chochote wanachokitaka hususani mambo ya uvunjifu wa sheria.

"Hawa bibi zetu wasiachiwe mzigo wa malezi kwasababu hawana uwezo  mkubwa wa kuwadhibiti vijana kimalezi, wazazi ambao tupo hapa tuache hii tabia ya kutua mzigo wa malezi kwa wazee wetu" alisema diwani huyo

Chengula alijitolea bati na mafundi wa kuezeka haraka nyumba hiyo na kukamilika pamoja na kumuwezesha bibi huyo vifaa vya kulalia na pesa ya chakula.

"Jamii yoyote lazima ijivunie uwepo wa kiongozi katika eneo husika,  kiongozi lazima usaidie watu wako na uwe mstari wa mbele kutatua matatizo ya wananchi wako usiku na mchana, Ukiwa kiongozi mzigo basi kubali kudharauliwa na waliokuamini na kukutuma uwe mwakilishi wao"alisema mh Nguvu Chengula.

Diwani huyo yupo tayari kumsaidia ujenzi wa nyumba nyingine kubwa na ya kisasa ili mradi aoneshwe kiwanja.


Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini