Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuunda Kamati Maalumu itakayochunguza tukio la kijana Musa Yahya ambaye anadai kupigwa na Polisi nakuingiziwa chupa sehemu za siri akiwa katika Kituo cha Polisi loliondo nakupelekea mguu wake kuoza akiwa kituoni.
Tukio hilo la kijana huyo, Mussa Yahya ambaye alikuwa na wenzake watano, wanatuhumiwa kuiba vitu vya wageni katika kambi ya kitalii iliyopo wilayani Ngorongoro Mkoani humo, na kupelekea kushikiliwa na askari polisi ambao wanalalamikiwa kuwapiga na kuwafanyia vitendo vya kikatili vilivyopelekea kuoza mguu wake wa kushoto, na kumfanya atembee kwa shida baada ya nyama za miguu kukatwa.
Akiwa katika ziara Wilayani Longido, na kufanya mkutano wa hadhara mjini Namanga, kijana huyo ambaye aliambatana na kaka yake, alimweleza Waziri Lugola katika mkutano huo, alipigwa na kuteswa kwa siku tisa huku yeye na wenzake wakiwa wamefungwa mikono na miguu huku wakiwa wanapigwa katika nyayo za miguu hadi kupelekea mguu wake kuoza.
“Nikiwa mimi na wenzangu, baada ya kuteswa na askari hao, tukapelekwa hospitali, na baada ya vipimo, ndipo mimi nikaambiwa na madaktari mguu wangu umeoza na wakakata nyama ya mguu wangu, nimepata mateso sana, pia walinifanyia ukatili sehemu za siri kwa kuniingizia chupa,” alisema Yahya.
Kufuatia malalamiko hayo pamoja na kaka yake Omary Yahya ambaye aliambatana naye katika mkutano huo wa Namanga, Waziri Lugola alimaliza ziara Wilayani Longido na kuelekea Wilaya ya Karatu na baadaye akafika Wilaya ya Ngorongoro mahali ambapo tukio hilo la kupigwa kwa kijana huyo lilitokea.
Akizungumza jana na mamia ya wananchi mjini Waso, Loliondo, Wilayani Ngorongoro, Lugola alisema kutokana kwa tukio hilo la kikatili lililotokea wilayani hapo, alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake kuhakikisha unafanyika uchunguzi huru ili haki itendeke kwani wananchi wamelalamika juu ya tukio hilo.
“Nilipata malalamiko haya nikiwa Namanga kutoka kwa aliyejeruhiwa, na nilimuona majeraha yake jinsi alivyokuwa ameteswa, hivyo basi ili nijue ukweli zaidi wa tukio hili, namuagiza Katibu Mkuu aunde Kamati kwa ajili ya kuchunguza kwa kina kuhusu tukio ili,” alisema Lugola huku akishangiliwa na mamia ya wananchi walihudhurika mkutano huo.
Lugola aliongeza kuwa, “Tunataka haki itendeke katika tukio hilo na matokeo yake yawe hadharani kwani hatuwezi kulalamikiwa tukaaa kimya na hata wale askari wachache ambao sio waadilifu wananchi watambue kuwa Jeshi la Polisi ni jeshi ambalo linaajiri vijana waliopata mafunzo ya kiweledi, wamefundishwa jinsi ya kukamata wahalifu, matumizi yapi yatumike endapo mtuhumiwa ameshindwa kutii agizo la polisi, sio kutumia nguvu kiasi ambacho kinaleta taharuki katika jamii, Kamati hiyo italeta majibu sahihi kuhusiana na tukio hilo,” alisema Lugola.
Lugola alisema, alishatoa maagizo kuwa, mahali popote polisi wakikutana na jambazi lenye silaha ya moto lazima askari ajihami kwa kupambana na jambazi huyo mwenye silaha, ili askari huyo asiweze akaja kupoteza Maisha wakati anacho kitu cha kujihami.
Lugola alifafanua kuwa, kuna makosa mengine ya kawaida kama hilo lililotokea katika kambi ya watalii huku akisema askari hawaruhusiwi kutumia nguvu zilizopita kiasi ikiwa kuleta vifo au na kuwasabishia wananchi majeruhi ya kudumu, hivyo alilitaka Jeshi la Polisi nchini wasiendelee kutumia nguvu kupita kiasi katika kushughulika na wahalifu popote pale.
Akasisitiza kuwa, endapo askari yoyote atakayebainika kutumia nguvu kupita kiasi na kuleta madhara, hafai na lazima atamchukulia hatua.
Lugola amemaliza ziara yake Mkoa wa Arusha ambapo alitembelea Wilaya zote akiangalia utendaji kazi wa Taasisi zake pamoja na kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa mara baada ya kuteuliwa kuwa Waziri, mwezi Julai mwaka jana.
Maagizo aliyoyatoa mara baada ya kuteuliwa, dhamana zitolewe saa 24, wananchi kutokubambikizwa kesi, pikipiki kuondolewa vituo vya polisi ambazo hazina sifa kuwepo katika vituo hivyo.
0 Comments