Na Greyson Mwase, Pwani
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka wachimbaji wa madini ya ujenzi aina ya kokoto katika mkoa wa Pwani kuwa na Mpango wa Ufungaji Mgodi utakaotumika kama mwongozo wa kuhakikisha mazingira yanaachwa yakiwa katika hali salama mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini hayo.
Profesa Kikula aliyasema hayo tarehe 21 Februari, 2019 katika nyakati tofauti alipofanya ziara yake katika migodi inayojishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini ujenzi aina ya kokoto iliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani yenye lengo la kutembelea wachimbaji wa madini hayo pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Profesa Kikula katika ziara hiyo akiwa ameambatana na Kamishna - Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki, wataalam kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ofisi ya Afisa Migodi Mkazi wa Lugoba pamoja na waandishi wa habari, Profesa Kikula alitembelea migodi ya Sisti Mganga, Gulf Concrete Company Limited na Yaate Company Limited iliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo.
Akizungumza katika nyakati tofauti mara baada ya kutembelea migodi hiyo, Profesa Kikula aliwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanakuwa na mipango ya ufungaji migodi mapema badala ya kusubiri mpaka shughuli za uchimbaji madini zinapomalizika hivyo kufanya zoezi la ufungaji wa migodi kuwa gumu huku wakiacha mazingira yakiwa hatarishi.
“Ninapenda kuwakumbusha kuwa suala la kuwa na Mpango wa Ufungaji wa Migodi ni la lazima kulingana na Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake, hivyo ninawataka kuhakikisha mnakuwa na mpango ili kuhakikisha mashimo hayaachwi wazi,” alisema Profesa Kikula.
Awali akiwa katika mgodi unaomilikiwa na Sisti Mganga Profesa Kikula alielezwa mafanikio ya mgodi huo ikiwa ni pamoja na kokoto za mgodi huo kutumika katika ujenzi wa daraja la Mto Wami uliopo mkoani Pwani, reli ya kisasa ya standard gauge na utengenezaji wa marumaru kwa ajili ya soko la ndani ya nchi.
Katika hatua nyingine Mganga alitaja changamoto zinazoukumba mgodi huo kuwa ni pamoja na tozo kubwa kutoka katika halmashauri na tozo nyingine zinazotozwa na kijiji cha Kihangaiko pasipo kuwa na risiti pamoja na ukosefu wa vifaa vya kisasa.
Profesa Kikula alisema kuwa, suala la tozo litafanyiwa kazi kwa kuliwasilisha mamlaka za juu kwa ajili ya kufanyiwa kazi na kusisitiza kuwa nia ya Serikali kupitia Tume ya Madini, ni kuhakikisha wachimbaji wa madini hususan wadogo wanafanya kazi katika mazingira mazuri yenye faida kubwa huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini pasipo vikwazo vyovyote.
Wakati huo huo, akiwa katika mgodi wa uzalishaji wa kokoto wa Gulf Concrete Limited Profesa Kikula alitoa mwezi mmoja kwa uongozi wa mgodi huo kuhakikisha wanarekebisha kasoro ya mazingira kwa kuhakikisha vumbi linalotoka wakati wa shughuli za uchimbaji wa kokoto halisambai kwani linaathiri wananchi wa vijiji vya jirani katika mgodi huo.
Alisema ni vyema wakazingatia Sheria ya Mazingira kwani vumbi mbali na kuathiri wananchi wanaoishi katika vijiji vya jirani linaweza kuathiri wafanyakazi wa mgodi huo.
Aidha, alituaka mgodi huo kuendelea kuhakikisha unatoa huduma kwa jamii inayozunguka mgodi huo na kutumia huduma za ndani ya nchi kama vile bidhaa pamoja na ajira kwa wazawa.
Katika hatua nyingine, Profesa Kikula akiwa katika mgodi wa kuzalisha kokoto wa Yaate Co. Limited, mbali na kuupongeza mgodi kwa kuaminiwa na kupewa kazi ya kusambaza kokoto kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya standard gauge unaotelekezwa na kampuni ya Yapi Merkezi na kutoa huduma mbalimbali kwa jamii inayouzunguka mgodi huo pamoja na ajira, aliutaka mgodi huo kuendelea kununua bidhaa/huduma kutoka kwa wananchi.
“Kutoa huduma bora kwa wananchi wanaozunguka mgodi kunaboresha mahusiano na kupunguza migogoro ya mara kwa mara inayoweza kujitokeza.
Awali akielezea mafanikio ya mgodi, Mkurugenzi Mtendaji wa Yaate Co. Limited, Eugen Mikongoti alisema mradi umenufaisha watanzania wengi kwa kuchangia maendeleo ikiwa ni pamoja na ulipaji wa zaidi ya shilingi bilioni 1.31 ambazo zimelipwa kama ushuru wa madini kati ya kipindi cha mwezi Juni, 2018 hadi Januari, 2019 na shilingi milioni 338.8 zilizolipwa kama mrabaha.
Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na utoaji wa fursa za ajira kwa watanzania hususan vijana wanaozunguka mgodi na kuziwezesha kampuni zinazomilikiwa na wazawa kushiriki katika miradi mikubwa hivyo kuzijengea uwezo wa kitaalam na kupata fursa.
Mikongoti alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuwezesha maendeleo ya wanachi wanoishi karibu na mgodi kupitia huduma za jamii ambapo mpaka sasa mgodi huo unaendelea na ujenzi wa nyumba za watumishi na kuhudumia wananchi katika zahanati iliyopo mgodini.
Katika hatua nyingine Mikongoti alipongeza kazi kubwa zinazofanywa na Tume ya Madini chini ya Mwenyekiti wake Profesa Kikula ikiwa ni pamoja na kuwatembelea, kuwapa elimu na kutatua changamoto mbalimbali.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) pamoja na Kamishna-Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki (katikati) wakiangalia moja ya bidhaa zinazotengenezwa na mgodi unaomilikiwa na Sisti Mganga uliopo katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani tarehe 21 Februari, 2019 ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya kokoto, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji. Kushoto ni mmiliki wa mgodi huo, Sisti Mganga.
Mmoja wa watendaji wa mgodi wa kuzalisha kokoto wa Gulf Concrete Company Limited, ulipo katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani, Ramesh Annlahamadu (kushoto) akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati) mara alipofanya ziara kwenye mgodi huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya kokoto, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji tarehe 21 Februari, 2019. Kulia mbele ni Kamishna – Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki.
Kwa Wale Wapenzi wa Nyimbo za Injili, Usipate Tabu!
Hii na Maktaba ya Nyimbo kutoka Tanzania na Afrika kwa Ujumla, Pakua Nyimbo za Injili Hapa Gospel Flavour
0 Comments