Waziri Kairuki Aitaka Tic Kuimarisha Huduma Za Mahala Pamoja

Waziri Kairuki Aitaka Tic Kuimarisha Huduma Za Mahala Pamoja

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji ) Angela Kairuki amekitaka Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC kupitia mfumo wa huduma za mfumo wa mahala pamoja kuboresha utoaji wa huduma kwa wawekezaji kupitia mfumo wa kielektroniki na kuwaagiza kuunganisha mfumo wa dirisha la uchakataji miradi (TIW) kwenye Kanda zote saba za kituo hicho Nchini ili kurahisisha mwenendo wa upatikanaji wa huduma  kwa wawekezaji.

Kairuki alisema mfumo huo unasaidia kuondokana na urasimu,ucheleweshwaji na unarahisisha upatikanaji wa leseni,cheti na  vibali ambao utasaidia kuongeza wawekezaji nchini ambapo kati ya kanda saba za TIC ni kanda moja tu ya Kaskazini ndio iliyoingizwa kwenye mfumo na kuagizwa kanda zingine ziharakishe mfumo huo ndani ya mwezi mmoja.

Waziri Kairuki aliyasema hayo February 20, 2019, baada ya kuzungumza na maafisa wanaotoa huduma ndani ya mfumo wa mahala pamoja na kufanya nao majadiliano juu ya namna ya kuboresha huduma hizo ambazo zinatolewa na taasisi 11 ndani ya jengo la TIC.

“Mfumo wa huduma za mahala pamoja ni mzuri sana, lakini tuhahitaji kuyafanyia kazi masuala kadhaa kwenye kila taasisi 11 zilizopo kwenye huduma za mahala pamoja ili kuondokana na changamoto ambazo zinachelewesha upatikanaji wa huduma za uwekezaji” alisema Kairuki.

Aidha aliwataka watendaji wa ardhi ndani ya kituo hicho kuweka vizuri takwimu za ardhi ya uwekezaji na kushughulikia changamoto za upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji ambao unasimamiwa na TIC.

Akiwa katika sehemu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Waziri Kairuki aliagiza  watendaji hao kuuona umuhimu wa utoaji wa cheti cha utambulisho wa namba ya mlipakodi  TIN kwenye Kituo hicho ili kurahisisha huduma kwa wawekezaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkurugenzi  wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bw. Geoffrey Mwambe alisema iwapo Serikali itawezesha taasisi zote zinazohusika na huduma za mahala pamoja kutoa huduma zake stahiki zinazohusu uwekezaji ndani ya ofisi za TIC itakuwa ni hatua kubwa katika uwekezaji.

“Taasisi zilizopo ndani ya mfumo wa mahala pamoja zinafanya kazi kubwa, tunachoomba sisi kama TIC ni kwamba huduma za taasisi hizo kwa wawekezaji zikamilike ndani ya TIC badala ya kwenda kwenye makao makuu ya ofisi hizo kufuata idhini ya vibali,leseni na vyeti husika kwa wawekezaji” alisema Mwambe.

Nae Kaimu  Mkurugenzi wa Idara ya huduma kwa wawekezaji Anna Lyimo alisema kwa sasa huduma za mahala pamoja zimekuwa na manufaa makubwa kwa wawekezaji kutokana na kuwapo kwa taasisi zote muhimu Kituoni na kwamba marekebisho yaliyotajwa na Waziri yatafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo.

“Tumeyapokea maagizo ya Waziri na tutayafanyia kazi, ni maagizo yenye tija kwa kituo” alisema Kaimu Mkurugenzi Idara ya  Huduma za Mahala Pamaoja wa TIC Anna Lyimo.

Huduma za mahala pamoja kwenye kituo cha uwekezaji Tanzania TIC zinajumuisha taasisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Taifa la usimamizi na uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA), Shirika la viwango Tanzania (TBS), Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na wenye ulemavu, Wizara ya Ardhi, Idara ya Uhamiaji,Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi (OSHA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA na Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA),

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini