AGPAHI YAWAPIGA MSASA WAIMARIKA TIBA SIMIYU


Afisa wa AGPAHI, Bw. Emmanuel Mashana, akiwezesha mada ya ufuatiliaji wa mahudhurio ya Waimarika Tiba CTC katika warsha iliyokutanisha Waimarika Tiba wa mkoa wa Simiyu ili kuwaongezea uweledi katika shughuli zao hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI.
Afisa wa AGPAHI, Bi. Harieth Novat, akiwaonyesha Waimarika Tiba rejesta za miadi ya WAVIU.
Maafisa wa AGPAHI, Harieth Novat (kushoto) na Emmanuel Mashana wakijadiliana jambo wakati wa warsha.
Washiriki wa warsha ya Waimarika Tiba Simiyu wakiendelea na zoezi la kujaza rejesta za miadi ya WAVIU.
Waimarika Tiba wakiwa kwenye kazi za vikundi katika warsha hiyo iliyoandaliwa na AGPAHI.
Waimarika Tiba wakiwa kwenye kazi  ya vikundi katika warsha hiyo iliyojumuisha  Vituo 36 vya kutolea huduma mkoani Simiyu huku wawezeshaji wakikagua ufanisi wa kazi.
Afisa wa AGPAHI, Bw. Emmanuel Mashana akiangalia kazi ya kikundi.
Asasi ya kitaifa inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), imewapiga msasa Waimarika Tiba wa mkoa wa Simiyu ili kuwaongezea uweledi katika shughuli zao hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI.

Waimarika Tiba ni Washauri nasaha wanaoishi na VVU ambao husaidia utoaji wa huduma katika vituo vya tiba na matunzo vilivyopo kwenye sehemu za kutolea huduma za afya.

Mratibu wa AGPAHI mkoa wa Simiyu, Bi. Dafrosa Charles, amesema ili kuwaongezea weledi Waimarika Tiba hao hivyo kufanya kazi zao kwa ufanisi, AGPAHI inaendesha warsha ya siku tano mjini Bariadi ili kuwapa stadi na mbinu mbali mbali.

Kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR) chini ya Vituo vya Udhibiti wa Magonjwa na Kinga (CDC), AGPAHI imekuwa ikiisaidia serikali katika kuboresha afya za wananchi hususan wale wanaoishi na VVU. Kwa sasa AGPAHI inafanya kazi katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Mwanza.

Katika warsha hiyo inayojumuisha vituo 36 vya matunzo na tiba kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Simiyu, Waimarika Tiba hao 39 wanakumbushwa kuhusu wajibu na majukumu yao katika kusaidia utendaji wa shughuli kwenye vituo vya kutolea huduma hizo hasa za ufuatiliaji wa watoro katika ngazi ya jamii.

Ili kuweza kufuatilia vyema watu wanaopata huduma za Tiba na Matunzo kwenye vituo vyao, Waimarika Tiba hao wamepimwa uelewa wao kuhusiana na ujazaji wa rejesta ya miadi kwa wateja wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV).

Lengo la zoezi hilo lililoongozwa na Maafisa wa AGPAHI, Bw. Emmanuel Mashana na Herieth Novati, lilikuwa ni kubaini mapungufu katika utumiaji wa rejesta hizo ili kuyashughulikia hivyo kuboresha upatikanaji wa taarifa.

Kufuatia mapungufu yaliyojitokeza maafisa hao kwa kushirikiana na Mratibu wa UKIMWI wa wilaya ya Bariadi, Bi. Joyce Mashauri, waliwaongoza Waimarika Tiba hao katika namna sahihi ya kujaza rejesta hizo kwa ufanisi wa ufuatiliaji wateja.

Aidha Waimarika Tiba hao walipitishwa kwenye ujazaji rejesta za miadi na ufuatiliaji wa watu wanaotumia huduma za VVU na UKIMWI. “Lengo la mazoezi haya ni kuhakikisha kuwa watakaporejea kwenye vituo vyao, kazi itafanyika kwa ufanisi kwa ufuatiliaji bora wa ufuasi wa huduma na tiba za VVU na upimaji wa wingi wa virusi katika damu,” amesema Bw. Mashana.

“Kwa kufahamu kuwa ugonjwa wa kifua kikuu umekuwa ukiwashambulia watu wengi hasa wenye VVU, Waimarika Tiba hao wamefundishwa kuhamasisha matumizi ya dawa za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kwa usahihi kama kinga kwa wanaostahili,”
amesema.

Masuala mengine ambayo Waimarika Tiba hao walifundishwa ni pamoja na kuhamasisha upimaji wa familia za wateja wa vituo vya tiba na matunzo na vipaumbele katika huduma ya VVU. “Ni matumaini yetu pia kuwa mtawahamasisha wanaume nao kupima. Uzoefu unaonyesha ni wanaume wachache tu wenye tabia ya kutafuta huduma za afya,” amesema Bi. Novati.


Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini