Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu 14 kwa tuhuma za makosa mbalimbali.
Mnamo tarehe 13.03.2019 majira ya saa 13:30 mchana huko Kitongoji cha Igadu, Kijiji cha Shuwa, Kata ya Iyunga – Mapinduzi, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya. TAMKA D/O MAMBA @ NGANGALE (28) Mkazi wa Kitongoji cha Masanga “A” aligundua kuuawa kwa mume wake aitwaye HADSON S/O HAIWOLE MWANGOKA (45) Mkazi wa Masanga “A” na mtu/watu wasiofahamika.
Marehemu aliondoka nyumbani tarehe 11.03.2019 saa 05:00 alfajiri kwenda shambani Kitongoji cha Igadu na hakurudi tena, harakati za kumtafuta zikaanza wakiwa wanamtafuta maeneo ya shambani kwenye korongo ndipo waliona kiganja cha mkono wa kulia kikiashiria kuna mwili wa marehemu umefukiwa.
Polisi walifika eneo la tukio na kukuta kiganja cha mkono korongoni na baada ya kufukua ulikutwa mwili wa marehemu aliyetambuliwa kuwa ni HADSON HAIWOLE MWANGOKA huku ukionekana kupigwa kitu kizito usoni. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali Teule ya Ifisi. Kiini cha tukio ni mgogoro wa ardhi/shamba la ukoo ambalo alikuwa analima marehemu ambalo linagombewa na wana ndugu baada ya baba yao kufariki dunia.
Watu nane wamekamatwa kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo ambao ni 1. PAULO HAIWOLE MWANGOKA (39) mchungaji na mkazi wa Kijiji cha Sanje 2. FREDRICK MOSES (36) Mkazi wa Iwindi 3. JOSHUA HAIWOLE (27) Dereva na mkazi wa Mlima reli 4. MICHAEL HAIWOLE (18) Mkazi wa Shuwa 5. ELIZABETH HAIBOLE (62) Mkazi wa Shuwa 6. JACOB S/O NOAH (51) Mkazi wa Izuo 7. ELIZA SHEYO (40) Mkazi wa Shua na 8. ERESIA HAIBOLE (64) Mkazi wa Shuwa. Upelelezi wa shauri hili unaendelea.
Mnamo tarehe 12.03.2019 majira ya saa 13:45 mchana huko Kitongoji cha Uzunguni, Kijiji cha Idimi, Kata ya Ihango, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya. Watoto wawili waliofahamika kwa majina ya 1. CLAVERY MASHAKA (05) na 2. GIFT MASHAKA (03) wote wakazi wa Idimi walifariki dunia baada ya kusombwa na maji ya mvua yaliyopita kwenye mfereji uliopo karibu na nyumba yao.
Chanzo cha tukio hili ni mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha na kutiririsha maji mengi yaliyosababisha vifo vya watoto hao.
Mnamo tarehe 13.03.2019 majira ya saa 15:00 Alasiri huko maeneo ya Mtaa wa Lusungo, Kata ya Itende, Tarafa ya Iyunga, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la EZEKIEL BONNY @ MWAKAPESA, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 28 – 30 na mkazi wa Itende alifariki dunia alipokuwa akiogelea kwenye mto Karabwe uliopo mtaa wa Lusungu.
Chanzo cha kifo chake inasemekana kuwa marehemu alikuwa na tatizo la ugonjwa wa kifafa ambacho kilimtokea akiwa anaogelea kwenye Mto huo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa tahadhari kufuatia matukio ya kufa maji yanayosababishwa na uzembe wa kutovaa maboya wakati wanapoingia majini, mtoni au ziwani. Aidha kufuatia mvua zinazonyesha nawasihi wazazi/walezi kuwa makini na watoto wao kwa kuweka uangalizi wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuwapeleka watoto wadogo Shuleni na kuwapokea ili kuwalinda dhidi ya madhara ya kutumbukia katika maji au kusombwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali.
Mnamo tarehe 13.03.2019 majira ya saa 10:45 asubuhi huko katika Kitongoji na Kijiji cha Matondo, Kata ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi wakiwa doria walimkamata JOHN RICHARD (24) Mkazi wa Kijiji cha Ifyenkenya akiwa na bhangi uzito wa gram 25. Mtuhumiwa ni muuzaji na mtumiaji wa bhangi.
Mnamo tarehe 13.03.2019 majira ya saa 12:00 mchana huko maeneo ya Sinde “B” Kata ya Sinde, Tarafa ya Iyunga ndani ya Jiji na Mkoa wa Mbeya, Polisi walimkamata ANATALIA MATUMLA (44) Mkazi wa Sinde “B” akiwa na pombe ya moshi lita 20 pamoja na mtambo wa kupikia pombe ya moshi. Mtuhumiwa ni muuzaji na mtumiaji wa pombe hiyo.
Mnamo tarehe 13 03.2019 majira ya saa 11:30 asubuhi huko maeneo ya Kata ya Ruanda, Tarafa ya Iyunga ndani ya Jiji na Mkoa wa Mbeya, Polisi walimkamata MAGRET KENYA (45) Mfanyabiashara na Mkazi wa Mwanjelwa akiwa na Pombe ya moshi lita18. Mtuhumiwa ni muuzaji na mtumiaji wa pombe hiyo.
Mnamo tarehe 13.03.2019 majira ya saa 12:00 mchana huko maeneo ya Ilolo, Kata ya Isanga, Tarafa ya Sisimba ndani ya Jiji na Mkoa wa Mbeya. Polisi walimkamata DORICE GEORGE (16) Mkazi wa Ilolo akiwa na mtambo wa kupikia pombe ya moshi. Mtuhumiwa ni mtengenezaji na muuzaji wa pombe hiyo.
Mnamo tarehe 13.03.2019 majira ya saa 14:30 mchana huko Kitongoji cha Mamba, Kijiji na Kata ya Mamba, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Polisi wakiwa doria walimkamata LUCY ISDORY (47) Mkazi wa Mamba akiwa na vipande15 vya nyama ya Pundamilia vyenye uzito wa kilogram 20 na Pombe Moshi lita 15 akiwa amehifadhi ndani ya nyumba yake. Upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao wa wawindaji haramu na kuwakamata.
Watuhumiwa wote watafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA
0 Comments