KADINALI ATUPWA JELA KWA KUNYANYASA KINGONO WAIMBA KWAYA


Mahakama Kuu nchini Australia imemhukumu Kardinali George Pell kifungo cha miaka sita gerezani, baada ya kukutwa na hatia ya kuwanyanyasa kingono wavulana wawili waliokuwa wakiimba kwaya katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrick, lililopo mjini Melbourne zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Jaji Mkuu wa Mahakama hiyo, Peter Kidd, alitoa hukumu hiyo jana kuwa Kardinali Pell atumikie kifungo cha miaka mitatu na miezi minane gerezani kabla ya kustahili kupatiwa msamaha.

Kardinali Pell, aliyekuwa Waziri wa Uchumi wa Vatican, alikutwa na hatia hiyo Desemba mwaka jana, kwa kumlawiti mvulana wa miaka 13 pamoja na mvulana mwingine pia mwenye umri wa miaka 13 mwishoni mwa miaka ya 1990.

Inaelezwa kuwa, tukio hilo lilitokea miezi michache baada ya Kardinali Pell kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Melbourne.

Pell, mwenye umri wa miaka 77, amekana mashtaka dhidi yake na Juni mwaka huu atakata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Hukumu hiyo imekuja zikiwa ni siku chache tangu Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, kutangaza vita kali dhidi ya watumishi wa kanisa hilo watakaobainika kujihusha na vitendo vya unyanyasaji.

Akifunga mkutano mkuu wa kanisa hilo mjini Vatican, kiongozi huyo alisema kwamba atazichukulia kwa uzito mkubwa kesi zote zinazowahusu viongozi hao na huku akiwaita wahusika kama watumishi wa shetani.

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini