MKURUGENZI WA LHRC KUPEWA TUZO YA MWANAMKE JASIRI DUNIANI


Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bi. Anna Henga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bi. Anna Henga ametajwa kama miongoni mwa wanawake 10 watakaotunukiwa tuzo ya Mwanamke Jasiri Duniani (International Women of Courage Award) 2019, tuzo inayoandaliwa na Ikulu ya Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa katika tovuti ya Ikulu ya Marekani, iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mike Pompeo, imesema kuwa watawatunuku tuzo wanawake 10 waliofanya mambo kwa ujasiri na uthubutu zaidi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.

Hafla ya utoaji tuzo itafanyika Machi 7, 2019 saa 4:00 Asubuhi kwa saa za Washington DC sawa na saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Mke wa Rais wa Marekani Bi. Melania Trump atakuwa mgeni rasmi.

Bi. Anna Henga ametajwa kama moja ya wanawake watakaotunukiwa tuzo hiyo kufuatia juhudi zake katika utetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania. Wanawake wengine tisa watakaotunukiwa tuzo hiyo wanatoka, Bangladesh, Burma, Djibouti, Egypt, Jordan, Ireland, Montenegro, Peru na Sri Lanka.

Tuzo ya International Women of Courage ilianzishwa mwaka 2007 kutambua mchango wa wanawake wanaojitoa kwa nguvu na ujasiri kama viongozi katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao bila kujali hatari ya maisha yao binafsi. Mpaka sasa, kupitia tuzo ya IWOC, Ikulu ya Marekani imetambua mchango wa wanawake zaidi ya 120 kutoka nchi zaidi ya 65 katika kutetea haki za binadamu, kudumisha asasi ya wanawake katika jamii na kudumisha amani na utawala bora katika nchi zao.

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini