Mwanasheria Wilaya Ya Makete Awaonya Wananchi Wanaojihusisha na UCHAWI Kwa Kizingio Kwamba Hakuna Sheria | ZamotoHabari.

Mwanasheria Wilaya Ya Makete Awaonya Wananchi Wanaojihusisha na UCHAWI Kwa Kizingio Kwamba Hakuna Sheria
Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe Godfrey Gogadi amewataka wananchi wilayani humo kuachana na vitendo vya kishirikina ili watumishi wa serikali wakiwemo waalimu waweze kufanya kazi zao.

Gogadi amesema ipo sheria ya uchawi hapa nchini na endapo itathibitika kwa mtu yeyote atachukuliwa hatua za kisheria na kuwaasa wananchi kuachana na vitendo hivyo ambavyo havina faida.

Vitendo vya kishirikina Vimekuwa vikiendelea katika baadhi ya vijiji  wilayani makete na kusababisha watumishi wakiwemo waalimu mara kwa mara kujikuta wakilala nje ya nyumba zao huku wengine wakiwakuta nyoka katika nyumba zao.

Katika Mkutano wa mkuu wa wilaya hiyo VERONICA KESSY na wananchi wa vijiji vya Mbalatse na Lupombwe,mwanasheria huyo ameamua kuwakumbusha wananchi uwepo wa sheria dhidi ya vitendo vya ushirikina pindi mtu yeyote atakapobainika.

“Ndugu zangu tunasheria yetu ya uchawi ambayo inakataza matendo haya na yale ni kosa la kijinai kwa hiyo msije mkafikiri kwamba kwenye uchawi hakuna sheria kama itathibitika pasipo shaka kuna mtu anajihusisha na haya maswala taratibu za kisheria zitachukuliwa, kwa hiyo ndugu zangu tubadilike kwa kuwa uchawi hauna faida na kama unafaida kwanini tusingefanya maji yafike huku”alisema Gogadi

Mkuu wa wilaya hiyo Mh Veronica Kessy amesema inashangaza mpaka sasa wananchi kuendelea kukumbatia vitendo hivyo ambavyo vinatia aibu wilaya ya Makete ndani na nje ya wilaya hiyo

“Mnanisikitisha na kudhihirisha kwamba kimaendeleo bado mkoa nyuma,kwa ustaarabu tu wenye michezo hii muiache kwasababu mnafahamika na wenzenu wanawafahamu na majina yenu tunayo na yule mama mmekataa kumrudisha sijui mlishamla nyama,watu wanakazana kuleta maendeleo lakini wengine wanaimani za kipepo tutapataje maendeleo”alisema VERONICA KESSY

Aidha amewaomba viongozi wa dini kukemea vitendo hivyo kwa kuwa moja ya kazi ya madhehebu ya dini ni kurekebisha mienendo ya waumini .

“Niombe sana madhehebu ya dini kila mtu anajua mungu yupo lakini wengine wanavibuli sasa wachungaji ndio kazi yenu tunawaomba sana maana hili linatuchafua Tanzania nzima ni Makete tunatia aibu”

Mmoja wa mwananchi aliyekuwepo kwenye mkutano huo amewaomba wananchi wenzake wanaofanya vitendo vya kishirikina kuviacha kwa kuwa havina faida yeyote huku akielezea machungu aliyonayo ya kumzika wifi yake aliyefariki dunia kwa kukatwa mapanga kwa madai ya kujiusisha na vitendo vya kishirikina.

“Kweli mimi naomba swala la uchawi kama kuna mtu yupo hapa naomba mviache kabisa, mimi hapa nilitoka juzi kisasapu msibani wifi yangu wamemkata na mapanga wanahisi alikuwa ni mchawi”alisema Mwananchi


Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini