Kutokana na kukua kwa Technolojia kila siku, na matumizi ya techolojia yanaongeza ufanisi, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umeanza na unaendelea na mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na mfumo wa kielektroniki wa kufuatilia na kuhifadhi taarifa za Hifadhi ya Taifa ya Chakula (Commodity Tracking System).
Lengo la kuwepo kwa mkakati huo ni kuongeza ufanisi kwa kupunguza mianya ya udanyanyifu na wizi na ili kufikia lengo hilo ifikapo mwishini mwa mwaka 2020, Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umekubali kusaidia kupata ufadhili wa fedha na utaalamu ili kufanikisha lengo hilo.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bi Vumilia Zikankuba wakati akizungumza kwa niaba ya watumishi wenzake Kwenye hafla ya kukabidhi mtambo wa kusafisha nafaka uliotolewa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na kuzinduliwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb).
Alisema kuwa WFP ni mdau muhimu wa NFRA katika kuzungusha akiba ya chakula huku Utekelezaji wa mauzo ya tani 36,000 ukiwa unaendelea.
Zikankuba alisema kuwa mpaka sasa Tani zote zimekwisha andaliwa na WFP wamekwisha kuchukua Tani 20,400 huku Tani 15,600 zikiwa zimekwisha andaliwa na zimehifadhiwa vizuri kwa ajili ya WFP kuchukua.
“Mauzo haya moja kwa maana yake ni kwamba Mkulima hasa mdogo anapata fursa ya soko la kimataifa moja kwa moja kwa kuwa NFRA hununua mazao yake moja kwa moja kutoka kwa wakulima” ,alikaririwa.
Bi Zikankuba alitumia mkutano huo kuujulisha ujumbe wa WFP kuwa NFRA ipo tayari na ina uwezo wa kuuza tani nyingine zaidi baada ya mkataba unaoendelea wa Tani 36,000 kukamilika.
“Pia tupo tayari kufanya mazungumzo na WFP ili kukusanya na kuwauzia mazao mengine ya nafakai mtama kuanzia msimu ujao wa mavuno”, alisema.
Aliongeza kuwa Mikakati na programu mbalimbali zinazoendeshwa na WFP zinasaidia NFRA kupata mazao yenye vigezo kupitia vikundi vya wakulima. Mfano: Katika msimu huu, kati ya vikundi vya wakulima 216 vilivyouza mahindi yao NFRA takribani vikundi 62 vilipata mafunzo ya kutunza na huhifadhi mazao ya nafaka kupitia programu ya Farm to Market Alliance ya WFP.
Na Mathias Canal, NFRA-Dodoma
0 Comments