Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameonya kuwa hatamvumilia kiongozi yeyote wa Mkoa, Wilaya ama Halmashauri ya Wilaya, Mji, Manispaa na Jiji atakayebainika kuhusika kuwatoza ushuru ama tozo yoyote wajasiriamali wadogo waliopatiwa vitambulisho.
Rais Magufuli ametoa onyo hilo wakati akizungumza na wananchi katika Mtaa wa Lumumba Jijini DSM, muda mfupi baada ya kutoka katika Ofisi Ndogo za Chama Cha Mapinduzi (CCM) alikoongoza kikao cha viongozi wenzake wa CCM.
Rais Magufuli amefafanua kuwa kiongozi yeyote atakayebainika kuwatoza wajasiriamali wadogo wenye vitambulisho atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuvuliwa madaraka, na hivyo ametaka wajasiliamali hao wasibughudhiwe.
Katika tukio hilo Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, akiwa na baadhi ya Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambao ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM Bashiru Ally Kakurwa, wamempokea Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward Lowassa ambaye ametangaza kurudi CCM ikiwa ni zaidi ya miaka mitatu tangu alipotangaza kujiunga na chama cha upinzani.
Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani, umoja, udugu na mshikamano na kujielekeza katika ajenda kuu ya ujenzi wa Taifa, badala ya kupoteza muda mwingi kwa marumbano yasiyo na tija.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA
0 Comments