RC Wangabo aonya vitendo vya Rushwa baraza la Ardhi Sumbawanga | ZamotoHabari

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametahadharisha vitendo vya kuchelewesha kusikiliza  mashauri mbalimbali katika baraza la ardhi na nyumba la Wilaya ya sumbawanga hali inayowapelekea wananchi kuhisi kuhusisha ucheleweshaji huo na vitendo vya rushwa na hivyo kuwataka kushikamana na kutafakari kauli mbiu ya wiki ya sheria yam waka huu iliyowataka kutoa haki kwa wakati kwa kushirikiana na wadau.

Amesema kuwa pamoja na mkoa kuwa na baraza moja la wilaya kati ya wilaya zake tatu na hivyo kupelekea kuelemewa na mashauri yanayotoka katika wilaya nyingine za mkoa hiyo isiwe sababu ya wajumbe wa baraza hilo kuchelewesha mashauri jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu.

“Najua kuna mzigo mkubwa na mlundikano wa kesi katika baraza, naambiwa kuna mashauri 399 na mengine 36 yamekaa zaidi ya miaka miwili, lakini pamoja na hayo wananchi nao wanlalamika kuhusiana na baraza la ardhi na nyumba Sumbawanga, moja ya malalamiko makubwa ni kwamba mashauri yanachelewesha ambapo wanachi wanaona kuna mashauri mengine yasingepaswa kuchukua muda mrefu na hili linaungana na lalamiko la pili ambalo linahusishwa baraza hili na vitendo vya Rushwa,” Alisema.

Ameyasema hayo katika hafla fupi ya kumuapisha mjumbe wa baraza la ardhi na nyumba la wilaya ya Sumbawanga Bi. Leticia Sami, ambapo kwa sasa Mkoa wa rukwa una baraza moja tu la ardhi na nyumba ambalo linapatikana katika wilya ya Sumbawanga.

Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Sumbawanga Bi. Frida Hamis Chinuku alisema kuwa mchakato wa kumpata mjumbe huo unaanzia kwa majina kupendekezwa na Mkuu wa Mkoa na kisha majina hayo kupelekwa kwa Waziri mwenye dhamana ambapo humteua mjumbe na hatimae mjumbe huyo kuapishwa.  

“Mjumbe yeyote kabla ya kuanza kazi anatakiwa kuapishwa na Mkuu wa mkoa katika Mkoa husika ambako baraza lipo, mchakato wa kumpata mjumbe huyu ulianza mwaka jana 2018 na aliteuliwa rasmi tarehe 5. July mwaka 2018 na kuapishwa leo. Kwa sasa baraza litakuwa na wajumbe jumla wanne japokuwa mjumbe mmoja ni mgonjwa,” Alisema.

Kiapo hicho kinatokana na maelekezo ya Kanuni za mwaka 2003 za Sheria ya namnba 2 ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya mwaka 2002.
 Bi Leticia Sami (kulia) akitia sahihi katika kiapo chake mbele ya mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) muda mfupi baada ya kula kiapo cha kuwa mjumbe wa baraza la ardhi na nyumba la Wilaya ya Sumbawanga.  
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. joachim Wangabo (kulia) akisalimiana na Mwenyekiti wa baraza la ardhi la Wilaya ya Sumbawanga  Frida Chinuku muda mfupi baada ya hafla ya kiapo cha mmoja wa wajumbe wa baraza hilo. 

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini