RIDHWANI PANGAMAWE ALIPENDA KINANDA AKIWA ‘KINDA’. | ZamotoHabari

Na Moshy Kiyungi

Mpenzi wa bendi ya msondo ngoma hupatwa na faraja kubwa pindi akimuona mwanamuziki Ridhwani Pangamawe, akiwa kashikilia gitaa jukwaani.


Wasifu wa Ridhwani unaeleza kuwa alianza kupiga muziki katika bendi ya Juwata, akiwa na umri mdogo wa miaka 15 mnamo mwaka 1979.

Muziki haukumuijia kama miujiza, ila yeye alizaliwa katika familia iliyokuwa ya wanamuziki.

Ridhiwan alinaeleza kwamba baba yake mzee Pangamawe alikuwa mwanamuziki katika bendi iliyokuwa maarufu pale Iringa mjini, iliyoitwa Highland Stars.Bendi hiyo ilitikisa mjini humo kwa muziki maridadi ilivyokuwa ikiporomosha, hasa mwishoni mwa miaka ya 1970.

Mazoezi ya wanamuziki wa bendi hiyo yalikuwa yakifanyika nyumbani kwao hata mama yake pia alikuwa anaweza kupiga gitaa.Pangamawe aliaanza kuonesha kipaji cha kupiga kinanda akiwa bado mdogo sana wa umri kama miaka mitano ambapo kaka yake Zuberi Pangamawe alimkuta kwa mara ya kwanza akipiga kinanda.

Alikiri kuupenda muziki tangia akiwa bado ‘Kinda’, alisema hata kaka yake, Zuberi, aliyekuwa mfanyakazi wa RTC pale Iringa, alikuwa anajua kupiga gitaa.Ridhiwani alisimulia kwamba kinanda hicho alikuwa akipenda kupiga kila aliporudi shule hata ule wakati wa mchana, alipokuwa akirudi kula chakula cha mchana, ilikuwa lazima aguse kinanda. Tabia ambayo hadi leo bado anapenda kufanya mazoezi sana.

Pangamawe baada ya kumaliza shule ya msingi Iringa, alikwenda jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya kuendelea na masomo ya sekondari.Wakati akiwa hapo Dar es Salaam, kaka yake aliwamtaarifu kuwa wajomba zake ambao ndio walikuwa wenyeji wake, akamwambia kuwa Ridhiwani ana uwezo wa kupiga kinanda.

Kipindi hicho hicho Waziri Ally ‘Kisinger’, alikuwa ameiacha bendi ya Juwata, nakarudi kwenye bendi yake ya awali ya The Revolutions sasa Kilimanjaro Band ‘Wana Njenje’.Bendi ya Juwata ikawa na pengo la mbofya kinanda kwakuwa takriban bendi zote kubwa zilikuwa na mpiga kinanda wakati huo.

Msondo walianza mkakakati wa kutafuta mpiga kinanda, ambapo wapiga vinanda kadhaa mashuhuri wa wakati huo walijaribu bahati zao kujiunga na bendi hii wakiwemo Kassim magati na hata Ally Tajruna ambaye alipigia bendi hiyo kwa mwezi mzima.

Wajomba zake Ridhwani, ambao walikuwa wapenzi wakubwa wa Msondo, wakiishi jirani na mzee Joseph Lusungu. Lusungu wakati huo alikuwa mmoja wa viongozi wa bendi hiyo ya Juwata na pia alikuwa mpulizaji hodari wa tarumbeta.Walimfuata mzee huyo na kumtaarifu kuwa wana mdogo wao ambae anaweza kupiga kinanda. Lusungu akawaeleza kuwa apelekwe kwa ajili ya usaili.

Ridhwani akakaribishwa Juwata ili kufanyiwa usaili chini ya msimamizi wa usaili wa mzee Kassim Mponda.Kwa kuwa hapo awali hakuwahi kugusa kinanda kinacho tumia umeme, hivyo alibabaika kidogo.Kabla ya hapo alikuwa akitumia kinanda cha kujaza upepo.Lakini hekima za mzee Mponda, zilitumika kwa kumuacha pasipo kumtilia maanani. 

wakati huohuo bendi ilikuwa ikifanya mazoezi ya wimbo wa “dunia uwanja wa fujo”. Hivyo mzee Lusungu akamuacha anaendelea kwenye chumba kimoja anapigapiga kinanda peke yake.Uhuru mkubwa alioupata ulimfanya awe jasiri akaanza kupiga nyimbo alizokuwa anazifahamu. Jambo hilo lililowavutia wanamuziki wenziwe waliomsikia kiasi cha kuacha mazoezi na kumfuata na kumtuza pesa.

Wakati huo haikuwa rahisi kutuzwa pesa kwa mwanamuziki mgeni ambaye alikuwa hajawahi hata kupigia bendi yoyote kabla ya pale, na tena wakiwa mazoezini.Mara moja wanamuziki walikubaliana kuwa ajiunge nao. Aliendelea kupiga nyimbo zilizoachwa na waziri, na kuchukuliwa rasmi kama mwanamuziki wa Msondo.

Jina la ‘Totoo’ alipachikwa kufuatia kwamba alikuwa bado mdogo ki umri na umbo. Wimbo wake wa kwanza kurekodi akipiga kinanda ulikuwa wimbo ‘Zhuleka’ utunzi wa Shaaban Dede.

Kwa bahati mbaya baada ya muda si mrefu kinanda kikaharibika na kwa muda wa zaidi ya miaka miwili akawa hapigi tena.Pangamawe akajiongeza kwa kuamua kuhamia kwenye upigaji wa gitaa. Alianza na kupiga second solo. Ujuzi wake mkubwa unasikika katika nyimbo za Kaka Selemani na Siwema.

Kisha akawa pia alipiga zito la besi, katika wimbo “Msafiri Kafiri”. Pamoja na kupiga gita hilo la besi, ilitokea wakati Kassim Mponda akaondoka katika bendi, wiki moja kabla ya siku ya kwenda kurekodi.Nafasi yake akakabidhiwa Ridhiwani Pangamawe kupiga gita la solo. Naye hakufanya ajizi, alizichambua nyuzi za gitaa hilo vizuri kabisa.

Kati ya nyimbo ambazo aliwahi kupiga anazozipenda zaidi mojawapo ni wimbo wa Queen Kasse.Hatimaye mwaka 1994, akaanza tena kupiga kinanda baada ya bendi kupata vyombo vipya. Akarekodi nyimbo kadhaa ukiwemo wimbo wa ‘Olee’.Kama alivyo kiongozi wa bendi hiyo Said Mabera, Ridhwani Pangamawe naye hajawahi kuodoa mguu wake kwenda katika nyingine, tangu alipojiunga nayo.

Pangamawe alisisitiza kuwa hana mpango wa kuhama kwa kuwa anaona hakuna sababu kubwa za msingi za kumfanya kuhama Msondo.

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini