Ruge Ananipigisha Stori Katikati ya Usingizi wa Mauti...."Nani Alitegemea Nitazikwa Kwa Heshima Hii" | ZamotoHabari.

RUGE ananiambia bila kufunua kinywa, akiwa kwenye usingizi wa mauti kwamba mtu anayeishi ndani ya mioyo ya watu ni mkubwa kuliko mwenye kujionesha na kujipa ufahari kwa watu.

Ananiambia kuwa umaarufu siyo kujiweka mbele kila wakati, unaweza kuwa daraja la wengine na utavuna kwenye jamii matunda yenye thamani.

Ruge ananiuliza: "Luqman, nani alitegemea ningezikwa kwa heshima hii?" Jibu langu ni "Hakuna Mkurugenzi". Ni kweli, wengi walimchukulia poa Ruge. Waliompa uzito, hawakufikiri kwamba alishasafiri ndani mno kwenye mioyo ya Watanzania.

Watanzania hawakupata nafasi ya kusema kabla ni kiasi gani walimpenda. Hakuwa na mikutano ya hadhara kusema wangejaa kwa wingi anapohutubia. Hakuwa mwanamuziki kusema wangenunua kwa wingi santuri zake. Si mcheza sinema, kwamba mauzo ya filamu zake yangedhihirisha mtaji mkubwa wa watu alionao.

Ruge ananiambia kuwa huhitaji vichwa vya habari uwe maarufu. Si mpaka uingie bungeni au uwe unakula kiyoyozi kwenye gari na ofisi ya waziri. La! Mtindo bora maisha wenye kuigusa jamii, unaweza kukufanya uwe lulu.

Tumewapoteza wanasiasa wangapi wakubwa lakini misiba yao haijagusa nyoyo kama Ruge? Wasanii wangapi? Ni kama Ruge ananiambia kuwa hata yeye mwenyewe hakujua kama anapendwa kwa kiasi kilichodhihirika baada ya umauti kumfika.

Ruge ananiambia kwamba huhitaji kuwa kiongozi wa kiroho ili ushike roho za watu. Viongozi wangapi wa kidini tumeshawazika lakini hawakutikisa kama Ruge inavyoifanya nchi yetu iwe na hekaheka?

Naona dhahiri Ruge anajaribu kuniambia maana halisi ya uongozi, kwamba si mpaka ugombee na uchaguliwe na wananchi au uteuliwe na Rais nafasi fulani serikalini. Uongozi ni vile unajichukulia.

Hakika! Ruge alijitafsiri kuwa ni kiongozi. Si uongozi wa Serikali, siasa au dini. Ruge aliamua kuwa kiongozi wa mtaa. Mitaa ikamuona ni kiongozi wao na ikamuelewa. Mitaa haikupaza sauti kumtangaza Ruge ni Kaka wa Taifa, bali walimhifadhi moyoni. Alipokufa, wameshindwa kuficha. Tumeona nguvu ya uongozi wa mitaa.

Ndimi Luqman MALOTO
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini