Serikali ya Zanzibar kujenga hospitali mithili ya Mloganzila | ZamotoHabari

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatarajia kujenga hospitali kubwa ya kisasa yenye uwezo wa kubeba vitanda 1,000 ili kutoa huduma pamoja na kufundishia watalaam wa fani mbalimbali za afya.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Bi. Asha Ali Abdulla alipotembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu juu ya uendeshaji wa hospitali hiyo.

Amesema ziara hiyo maalum imefanyika kufuatia agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein la kuwataka watendaji wa Wizara ya Afya Zanzibar kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mloganzila ili kupata uzoefu wa uendeshaji wake katika nyanja za tiba na mafunzo kwa watalaam walioko kwenye mazoezi kwa njia ya vitendo. 

Amesema ujenzi wa hospitali hiyo ya kisasa mithili ya Hospitali ya Mloganzila utaanza katika mwaka huu wa fedha 2019/2020 na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo imelenga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma kwani kwa sasa wananchi walio wengi wanategemea Hospitali ya Mnazi Mmoja yenye vitanda 776 ambayo imezidiwa wingi wa wagonjwa

“Tumekuja kujifunza kwenu kwakua mna uzoefu mkubwa wa kuendesha hospitali kubwa kama hii na sisi tunahitaji kujipanga, kujifunza na kupata uzoefu wa kutosha kutoka kwenu ili hospitali yetu ikikamilika tuweze kuiendesha vizuri kama ambavyo wenzetu mnafanya” amesema Abdulla.

Hospitali hiyo itajengwa katika eneo la Binguni wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja ambapo ujenzi huo utafanyika kwa awamu kulingana na rasilimali zinavyopatikana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru ameahidi kutoa ushirikiano na uzoefu wa kila aina ili kuhakikisha lengo la ujenzi wa Hospitali hiyo unafanikiwa.
  Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Asha Ali Abdulla (aliyevaa mtandio wa bluu) akizungumza na viongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila na Upanga mara baada ya kuwasili Mloganzila kwa ziara maalum ya kujifunza. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili Prof. Lawrence Museru.
 Mhandisi wa mitambo katika Hospitali ya Mloganzila Bw. Akaniwa Msengi (kushoto) akielezea jinsi mitambo ya hewa safi inavyofanya kazi.
 Watendaji wa Wizara ya Afya Zanzibar wakiendelea kupata maelezo ya kina juu ya mitambo mbalimbali inavyofanya kazi hospitalini hapo.
  Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya ndani na wagonjwa wa nje Dkt. Rose Minja (aliyevaa koti jeupe) akitoa maelezo ya huduma zinazofanyika katika idara hiyo.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Asha Ali Abdulla (katikati) pamoja na Mhandisi Cosmas Masolwa wakipatiwa maelezo na Msimamizi wa kitengo cha kusafisha damu kwa magonjwa ya figo Bw. Emanuel Mlay (kushoto) kuhusu huduma ya kusafisha damu inavyotolewa hospitalini hapo.
 Kaimu Meneja wa maabara Mloganzila Esuvat Moses (kulia) akifafanua namna maabara inavyofanya kazi, vipimo vinavyotolewa pamoja na aina ya mashine zilizopo katika maabara hiyo.
 Daktari Bingwa wa magonjwa ya dharura katika Hospitali ya Mloganzila Henry Sawe (kushoto) akiwaelezea watendaji wa Wizara ya Afya Zanzibar jinsi huduma za dharura zinavyofanyika hospitalini hapo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Asha Ali Abdulla (wa nne kutoka kushoto kwa walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wizara hiyo na wa Muhimbili, kulia kwakwe ni Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru akifuatiwa na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mloganzila Dkt. Julieth Magandi.

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini