Spika Za Masikioni Chanzo Cha Matatizo Ya Usikivu | ZamotoHabari.

Spika Za Masikioni Chanzo Cha Matatizo Ya Usikivu
Spika za masikioni maarufu kwa jina la “Headphones” zimetajwa kuwa chanzo kinachopeleka tatizo la usikivu hafifu kwa watu.

Hayo yamesemwa jana na Waziri mwenye dhamana ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza na wananchi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Jijini Dar Es Salaam katika kuadhimisha siku ya usikivu duniani.

Waziri Ummy amesema kuwa matumizi ya simu za kisasa yameongeza kasi ya watu kutumia spika za masikioni jambo ambalo linahatarisha kuwa na watu wengi wenye matatizo ya usikivu.

“Unakuta kijana kuanzia asubuhi mpaka jioni ameweka spika za masikioni anasikiliza muziki hawajui wanajiweka katika hatari ya kupata tatizo la usikivu” amesema Waziri Ummy na kuendelea kusema kuwa kundi la vijana liko hatariki kupata matatizo ya usikivu.

Waziri Ummy ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kupunguza matumizi ya spika za masikioni ili kuweza kujikinga na matatizo ya usikivu.

“Nitoe rai kwa vijana wapunguze matumizi ya spika za masikioni kwa muda mrefu, tusipo kuwa makini tunaweza kujikuta tuna taifa lenye watu wengi wenye matatizo ya kutosikia vizuri” amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa tatizo la usikivu hutokea pia kwa njia mbalimbali ikiwemo kwa kuzaliwa na tatizo hilo au kulipata ukubwani kutokana na sababu nyinginezo ambazo zinaambata kwa kukaa kwa muda mrefu kwenye sehemu zenye kelele nyingi pamoja matatizo yanayoambata na afya ya sikio.

Waziri Ummy amesema kuwa ni jambo jema kuona sasa matibabu ya matatizo ya usikivu hafifu yanapatikana hapa hapa nchini huku akiwataka wananchi kukata bima za afya ili kuweza kupata matibabu kwa uhakika.

“Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha tatizo hili linazuiliwa kabla ya kutokea lakini pia kuhakikisha matibabu yanapatikana yakiwemo kutumia mashine ya mawimbi ya sauti, upasuaji wa kuziba tundu la ngoma ya sikio pamoja na kupandikizwa vifaa vya kusaidia kusikia” amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo alisema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2018 Hospitali ya Muhimbili imefanikwa kuwapatia wagonjwa 116 vifaa vya mawimbi ya sauti, wagonwja 43 walifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu la ngoma ya sikio.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa na kuhakikisha matibabu yanapatikana hapa hapa nchini.

Awali akitoa taarifa yake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Bw. Makwaiya Makani amesema kuwa wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali katika eneo la usikivu ikiwemo kutoa huduma ya upandikizaji vifaa vya usikivu kwa Watoto wenye matatizo ya hayo.

“Tangu mwezi Juni mwaka 2017 tayari watoto 21 wamepandikizwa vifaa vya usikivu kitaalam kwa jina la ‘cochlear implants” amesema Bw. Makani

Bw. Makani amesema kuwa wameendesha kliniki ya siku mbili katika Hospitali ya Mloganzila kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya matatizo ya usikuvu ambapo watu 264 wamejitokeza kati yao watu 172 walihitaji uchunguzi zaidi wa usikivu, watu 64 wamekutwa na matatizo ya usikivu na tayari wamepatiwa rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi na watu 31 wamekutwa na nta za masikioni,pia watu 26 wamekutwa na maambukizi kwenye masikio ambao wamepatiwa rufaa ya matibabu zaidi.

Tatizo la usikivu linazidi kuongezeka siku hadi siku. Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 5 ya watu duniani wana tatizo la usikivu. Tatizo hili litaongezeka maradufu kila mwaka. Inatakiwa kila mmoja achukue hatua kujikinga na tatizo hili ikiwemo kuepuka sehemu zenye kelele na pia kusikiliza mziki kwa sauti kubwa na kwa muda mrefu na kwa kutumia spika za masikioni.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini