TANZANIA YAPIGA HATUA UWEZESHAJI WANAWAKE | ZamotoHabari

Na Mwandishi Wetu – New York Marekani
Tanzania ni nchi mmojawapo duniani iliyofanikiwa kupiga hatua katika kuwawezesha wanawake kijikwamua kiuchumi kwa kuwasaidia kupata mikopo isiyo na riba inayowawezesha kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.

Hayo yamesemwa leo na Mh Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, katika Mkutano Mkuu wa 63 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea New York, Marekani.

Waziri Ummy alieleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fursa za mikopo na kufanyia marekebisho Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 2018 ambayo imefuta Riba kwa mikopo yote inayotolewa kwa wanawake kupitia Halmashauri.

Alisema Halmashauri zimekuwa zikichangia asilimia 5 ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, matokeo yake kiwango cha fedha zinazotolewa na Halmashauri kwa ajili ya mikopo ya wanawake kimeongezeka kutoka bilioni 3.4 mwaka 2015/16 kufikia bilioni 16 mwaka 2017/18. 

Waziri Ummy alieleza kuwa tangu mwaka 2015 Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kutoa elimu bure ya Msingi na Sekondari na kufanya ongezeko la asilimia 80 katika uandikishaji wa watoto wa shule za msingi na ongezoko la asilimia 20 kwa Sekondari. 

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bila vikwazo vyovyote mwaka 2018 Serikali imefuta tozo ya kodi katika taulo za kike (pads) na hivyo kupelekea upatikanaji wake kuwa rahisi na kwa gharama nafuu ambapo mwanzo watoto wengi wa kike walikuwa wanakosa vipindi madarasani kutokana na kukosa taulo hizo.

Katika huduma za afya, Tanzania imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za afya hususan huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na maboresho ya miundombinu ya afya na chanjo. Kwa mwaka 2018/19 Kati ya vituo vya afya 518, vituo 304 vimekarabatiwa ili kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji na hivyo kuwa na jumla ya vituo 459 nchi nzima vinavyotoa huduma za dhalura na uzazi ukilinganisha na vituo 109 mwaka 2015.

Na katika sekta ya nishati Waziri Ummy alieleza kuwa Tanzania kupitia mradi wa umeme vijijini (REA) imeweza kusambaza umeme katika vijiji zaidi ya 7000 kati ya vijiji 15000 sawa na asilimia 46 ya vijiji vyote nchini hili limesaidia sana kuwawezesha wanawake kupata fursa mablimbali kutokana na upatikanaji wa nishati hiyo kwa urahisi kuanzisha miradi ya kiuchumi ikiwemo viwanda vidogo vidogo.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Taarifa ya Utafiti wa Upatikanaji wa Nishati Tanzania ya mwaka 2016 asilimia 32.8 ya kaya Tanzania bara zina Umeme, na asilimia 44.2 Zanzibar. Upatikanaji wa umeme umewezesha huduma za afya kupatikana kwa wepesi hasa huduma za uzazi, upatikanaji wa maji na kurahisisha shughuli zingine za uzalishaji mali kwa wanawake.

Mkutano wa 63 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa wa Hali ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2019 unaendelea jijini New York Nchini Marekani ukiwa na Kaulimbiu inayosema "Mifumo ya Hifadhi ya Jamii, Huduma za Umma na Miundombinu Endelevu kwa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake na Wasichana".
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Kushoto) akiwa katika katika Mkutano Mkuu wa 63 Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea katika jiji la New York nchini Marekani.

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini