Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu
Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu amejitokeza na kumtakia heri Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa kufuatia uamuzi wake wa kurejea Chama Cha Mapinduzi.
Lowassa ametangaza kurejea CCM mapema Machi 1, 2019 ambapo alipokelewa na Mwenyekiti wa Chama hicho Dkt, John Pombe Magufuli katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho yaliyopo Lumumba Jijini Dar es salaam.
Lissu ameandika, "Edward Lowassa mwenyewe amesema amerudi nyumbani, maana yake ni kwamba alikuwa 'ugenini' tangu Julai 2015. hakuwahi kutuhonga wala kununua chama chetu kama tulivyotukanwa huko nyuma".
"Tulimkaribisha na kumpatia majukumu ya kutuongoza kwenye mapambano ya 2015. na alitekeleza majukumu hayo vizuri kwa kadri alivyoweza, na kadri tulivyomwezesha. matunda ya kazi yake, na ya kazi yetu yanajulikana", ameandika Lissu.
Lissu ameongeza kuwa, "na pengine sasa wataacha kumtishia kumnyang'anya mafao yake ya kisheria kama Waziri Mkuu mstaafu, badala ya kumlaani kwa kuondoka kwetu 'ugenini', mimi namtakia kila la kheri na mapumziko mema 'nyumbani' kwake sisi tutaendelea na safari yetu ya Canaan".
Wakati akipokelewa na uongozi mkuu wa CCM, Lowassa mwenyewe hakubainisha nini sababu ya kurejea CCM, bali aliishia kusema kuwa amerudi nyumbani.
0 Comments