WATATU WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA WIZI MTANDAONI

Na Tiganya Vicent, Tabora
Watu watatu wanaotuhumiwa kujihusisha na wizi wa mitandaoni wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora wakikabiliwa na tuhuma nne.

Shauri hilo la uhujumu uchumi linawakabili Rajab Said Makwaya, Rashid Idd Kayombo na Said Shaban Issa wote wakazi wa Manispaa ya Tabora.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Tito Mwakalinga ulidai mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa wa Tabora, Chiganga Mashauri kuwa, watuhumiwa walitenda makosa hayo kati ya Februari 23 hadi 24 mwaka huu.

Wakili Mwakalinga aliieleza Mahakama hiyo kuwa, kila mtuhumiwa anakabiliwa na makosa mawili ya kukutwa na mali inayodhaniwa imepatikana isivyo halali pamoja na kutengeneza mpango wa kitapeli ili kujipatia fedha kupitia mtandao.

Ilidaiwa kuwa, mnamo Februari 24 mwaka huu Mtaa wa Kariakoo, Manispaa ya Tabora watuhumiwa walikutwa wakimiliki nyumba moja kila mmoja zikiwa na thamani ya jumla ya shilingi milioni 105 ambazo walizipata kinyume cha sheria. 

Siku hiyo mtuhumiwa Rajab Makwaya alikutwa akimiliki nyumba yenye thamani ya milioni 35, Rashidi Issa akimiliki nyumba ya milioni 30 na Said Shaban anamiliki nyumba ya milioni 40.

Wakili Mwakalinga alidai katika shitaka la nne kuwa kati ya Februari 23 hadi 24 mwaka huu watuhumiwa walitengeneza mpango wa udanganyifu wa kujipatia fedha kupitia mitandao ya simu.

Aliongeza kuwa kwa kupitia mtandao wa simu waliweza kumdanganya Zengwe Josephine na kujipatia shilingi milioni mbili kinyume na kifungu cha 6(b) na kifungu namba 57(1) na 60 cha sheria ya uhujumu uchumi iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Watuhumiwa hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo na walipelekwa rumande hadi leo kesi yao itakapotajwa tena.

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini