WAZIRI BITEKO AZINDUA BODI YA GST,AITAKA KUIWEZESHA GST KURAHISISHA MAISHA YA WACHIMBAJI | ZamotoHabari

Asteria Muhozya na Samwel Mtuwa, Dodoma
Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), imetakiwa kuiwezesha taasisi hiyo kurahisisha maisha ya Wachimbaji Wadogo, wa Kati na Wakubwa kwa kuhakikisha wanapata taarifa za tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akizundua Bodi ya GST na kueleza kuwa, shughuli za utafiti ni moja ya maeneo muhimu katika sekta ya madini kutokana na kutoa uhakika kwa wachimbaji na hivyo kukidhi matarajio ya wadau.
Pia, ameitaka bodi kuiwezesha taasisi hiyo kutoa ubunifu mpya utakaowezesha taasisi hiyo kuongeza mapato kwa serikali kutokana na shughuli na huduma zinazotolewa na GST.
Katika hatua nyingine, Waziri Biteko ameitaka bodi hiyo kuhakikisha GST inapata Ithibati ya maabara yake ikiwemo kutangaza huduma zinazotolewa na maabara hiyo ili kuwawezesha wadau kuifahamu na kuitumia.
Aidha, ameitaka bodi husika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sera, sheria na taratibu zilizowekwa na kueleza kwamba, taasisi hiyo inao watendaji wazuri wa kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kiamilifu na kutumia fursa hiyo kumpongeza Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST Yokberth Myumbilwa, kwa kusimamia vema utendaji wa GST.
Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema taasisi hiyo ni kitovu cha sekta ya madini nchini na kwamba ndiyo imeshikilia mstakabali wa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.
Ameongeza kuwa, bado yapo majukumu ya taasisi hiyo ambayo hayajafanikiwa na hivyo kuitaka bodi hiyo chini ya Prof. Ikungula kuhakikisha yanafanikiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Justinian Ikingura amesema bodi hiyo inatambua umuhimu wa rasilimali madini katika kuchangia pato na kukuza uchumi wa taifa ikiwemo kutambua nia na lengo la Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.
Amesema ili kufikia lengo hilo, ni muhimu GST ikawezeshwa ipasavyo kupitia wizara ili iongeze kasi na tija zaidi katika kutekeleza majukumu yake, hususan katika maeneo ya kufanya utafiti na kukusanya taarifa muhimu za kijiosayansi za kubaini maeneo yenye miamba yenye vishiria vyakuwepo madini ya kimkakati yanayohitajika zaidi katika matumizi ya teknolojia ya viwanda vya kielekitroniki, zana za utafiti wa mawasala ya anga na matumizi maalum katika viwanda vingine, ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchini katika maeneo hayo. 
“Kwa mfano madini lithium, cobalt na palladium yanazidi kupata umuhimu wa pekee katika matumizi ya viwanda vya kimkakati. Hivi majuzi takriba wiki moja iliyopita bei ya Palladium ilifikia kiasi cha dola za kimarekani 1,600 kwa wakia na kuzidi hata dhahabu ambayo ikiwa karibu dola 1,300 kwa wakia moja. Lakini si wengi wanatambua madini ya Palladium ambayo yako katika kundi la metali za Platinum, yaani Platinum Group Metals (PGM),” amesisitiza Prof. Ikingura.

Ameongeza kuwa, eneo jingine ni uboreshaji wa huduma za maabara za uchunguzi na upimaji wa miamba na madini yake ili zikidhi viwango vya kimataifa, na hivyo kuvutia wawekezaji katika sekta ya madini kutumia zaidi maabara za ndani ya nchini badala ya kupeleka sampuli katika maabara za nje ya nchi, na hivyo kupoteza fedha za kigeni.

Vilevile, amesema ipo haja ya kuboresha na kuongeza thamani taarifa za jiofikizia na jiokemia zilizo katika hifadhi au kanzidata ya GST ili ziweze kuwa na thamani kubwa zaidi  kwa taifa na kwa wawekezaji katika sekta ya madini, suala ambalo  litaiweesha GST kuongeza maduhuli ya serikali kupitia wizara.

Mbali ya Mwenyekiti, wajumbe wa bodi hiyo ni Abdulkarim Hamisi Mruma, Emanuel Mpawe Tutuba, Bibi Bertha Ricky Sambo, Shukrani Manya, David R. Mulabwa na Bibi Monica Otaru.

Bodi hiyo imezinduliwa Machi 27, 2019 Makao Makuu ya GST, jijini Dodoma.
 Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Wajumbe wa  Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti  wa  Madini Tanzania (GST), Watendaji wa wizara  pamoja na watumishi  mbalimbali kutoka  GST wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Bodi ya GST uliofanyika jijini Dodoma tarehe 27/3/2019.
 Waziri wa Madini Doto Biteko,  akimkabidhi  kitendea kazi mmoja wa wajumbe wa Bodi ya GST , Kamishna wa Madini, David Mulabwa wakati wa uzinduzi wa bodi. Anayeshuhudia kulia ni Mwenyekiti wa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan  Kitandula.
 Waziri wa Madini Doto Biteko (kushoto) akizungumza na jambo wakati wa uzinduzi wa bodi ya GST .kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya GST Prof. Justinian Ikingula.
Waziri wa Madini Doto Biteko akimkabidhi moja a kitendea kazi mjumbe wa Bodi ya GST Prof. Shukran Manya wakati wa Uzinduzi wa Bodi ya GST uliofanyika tarehe 27/3/2019 katika ukumbi wa mikutano wa wizara , pembeni anayeshuhudia makabidhiano hayo ni mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Justinian Ikingula.
 Waliokaa kutoka kushoto ni  Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya  Bunge ya Nishati na Madini  Dustan  Kitandula, Waziri wa Madini Doto Biteko , Mwenyekiti wa Bodi ya GST Prof. Justinian Ikingula, na Naibu waziri wa Madini Stanslaus Nyongo. Wengine katika picha waliosimama ni Wajumbe wa Bodi ya GST na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya GST. 

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini