Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa –TAMISEMI, Mhe. Seleman Jafo, amefanya ziara mkoani Singida ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Singida ambapo amewapongeza viongozi wa Serikali ya mkoa kwa kuanza ujenzi wa hospitali hiyo kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma za afya.
Waziri JAFO ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea ujenzi wa hospitali hiyo inayojengwa katika kijiji cha Sokotoure kata ya Ilongero mkoani Singida na kusisitiza kuwa ziara yake hiyo ililenga kuzihamisha fedha hizo kwenda halmashauri ya Ikungi kama angekuta ujenzi wa hospitali hiyo hujaanza.
“Leo nimekuja kuwatembelea kwa ajili ya kuja kuangalia ujenzi huu, Mhe. RC naomba nikwambie, nilikuja kuhamisha hizi fedha ndio agenda niliyokuja nayo. Nilikuja hapa kutoa maelekezo ya kiserikali hizi fedha ziende Halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Laiti kama ningekuja hapa ningekuta hizi fedha bado hamjaanza ujenzi.
Lakini niwapongeze sana kwa kukuta hii kazi imeanza, na hili ndio Mheshimiwa Rais analihitaji. Ametenga fedha Bilioni 1.5 kwa lengo la kuhudumia wananchi wake sio jambo lingine.
Amesema kwa sababu Serikali imeshatoa fedha zote kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo, hivyo amewataka watendaji wa Halmashauri pamoja na watendaji wa Sekretalieti ya mkoa kushirikiana kwa pamoja ili kukamilisha ujenzi huo wakati.
“Tunajenga hospitali 67 ni mapenzi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli”. “Mheshimiwa RC, Dkt. Rehema Nchimbi, mimi hapa leo nimefurahi sana. Endeleeni na jambo hili”.
“Maelekezo yetu ni kwamba inapofika tarehe 30 mwezi Juni, 2019, hii awamu ya kwanza inatakiwa ikamilike kwa asilimia zote 100”.
“Binafsi nimeridhika sana hospitali inajengwa ili wananchi wapate huduma”.
“Leo siku yangu mmenifanya nisizeeke” Waziri Jafo amemalizia kwa furaha.
Kwa upande wao, Viongozi wa Mkoa wa Singida wamemshukuru Waziri Jafo kwa ziara yake hiyo yenye kuleta hamasa na nguvu kwa wananchi wa mkoa wa Singida hasa wa halmashauri ya Singida katika ujenzi huo wa hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Singida.
Aidha wameishukuru Serikali ya awamu ya Tano kwa kuwapatia fedha bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa dhati katika kuisimamia hadi itakapokamilika kwa muda uliopangwa.
Nao, Wananchi wa kata ya Ilongero wamesema ujenzi wa hospitali hii utawaondolea kero ya muda mrefu ya kufuata huduma ya afya katika maeneo ya mbali.
Katika hatua nyingine, Waziri Jafo ametembelea shule ya sekondari ya Ilongero ili kujionea miundombinu ya shule hiyo kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri.
Pia akapata muda wa kuzungumza na walimu pamoja na wanafunzi ambapo amewata wanafunzi hao kutumia muda wao mwingi katika kujifunza mambo ya darasani ili kufauli mitihani yao.
Waziri Jafo amendelea na ziara yake katika mkoa wa Tabora, lengo ni ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo iko chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa –TAMISEMI
MATUKIO KATIKA PICHA
Ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida ukiendelea
Mheshimiwa Mbunge wa Singida Kaskazini Mhe. Monko Justine Joseph (wa kwanza kushoto) akizungumza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa –TAMISEMI, Mhe. Seleman Jafo, akizungumza na wananchi katika kijiji cha Sokotoure kata ya Ilongero mkoani Singida wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya wilaya Singida, mkoani Singida.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa –TAMISEMI, Mhe. Seleman Jafo, (wa pili kushoto) mara baada ya kuwasili katika viwanja vya shule ya sekondari Ilongero mkoani Singida.
0 Comments