Ahukumiwa Miaka 30 Jela Kwa Kumbaka Mwanafunzi na Kumpa Ujauzito | ZamotoHabari.

Ahukumiwa Miaka 30 Jela Kwa Kumbaka Mwanafunzi na Kumpa UjauzitoMahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, imemhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 12 mfanyabiashara Anthony Mandawa (58), baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mwanafunzi na kumsababishia ujauzito.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, Rashid Chengula, alisema Mandawa alitenda kosa hilo Februari mwaka jana na mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Hakimu Chengula alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliyekuwa akisoma shule ya Upili Samora na kumsababishia ujauzito huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Alisema Jamhuri kupitia mashahidi wake, akiwamo muathirika wa tukio hilo bila kuacha shaka, mfanyabiashara amefanya makosa yote mawili hivyo kumtia hatiani na kumpatia hukumu hiyo.

Awali katika utetezi wake, mshtakiwa Mandawa alikana kutenda kosa hilo, huku akikosoa mwenendo wa shauri hilo kwa madai kuwa muathirika alichelewa kutoa taarifa akidaiwa kuripoti baada ya siku 30.

Aidha, alidai kuwa yeye (mshtakiwa) ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi na kujitetea kuwa mwanafunzi anayedaiwa kubakwa hajaathirika hivyo mahakama inathibitishaje kama kweli alimbaka.

Hata hivyo, mahakama ilisema utetezi wa mshtakiwa hauna mashiko ya kutomtia hatiani.

Shauri hilo lilikuwa likiendeshwa na mawakili wawili wa serikali, Davice Msanga ambaye aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa Mandawa, ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Isanga, alishtakiwa na Jamhuri kwa makosa mawili ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha kwanza kinyume na kifungu namba 130 (2) e na 131 (1) ya kanuni ya adhabu.

Kosa la pili ni kumsababishia ujauzito mwanafunzi huyo, kinyume na kifungu namba 60 A (3) cha Sheria ya Elimu sura ya 353 na marekebisho yake kifungu namba 22 (3) cha sheria namba 2 ya mwaka 2016.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Chengula, alisema mshtakiwa anahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 12 kwa kosa la kwanza ikiwa ni pamoja na kulipa faini ya Sh.milioni mbili.

Kosa la pili mtuhumiwa huyo alihukumiwa kutumikia jela miaka 30 kwa kosa la kumsababishia ujauzito mwanafunzi huyo, ambaye pia amemsababisha akatishe masomo yake na vifungo hivyo aliviamuru kwenda pamoja.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini