Haikuwa sikukuu ya wajinga kama ambavyo mashabiki wa rapa Nipsey Hussle walitamani iwe ili taarifa za kifo chake zibaki kuwa za uongo. Lakini ilikuwa kweli, rapa huyo alipoteza uhai baada ya risasi mbili kutua kichwani na tumboni mwake.
Kwa mashabiki wa kazi zake, hakuwa rapa tu bali mwanaharakati aliyepambana kuhakikisha usawa hasa kwa Wamarekani wenye asili ya Afrika unakuwapo.
Jana akiwa nje ya duka lake la mavazi Marathon Clothing rapa huyo alivamiwa na kushambuliwa kwa risasi nyingi na mbili zilimpata kichwani na tumboni na kukatisha safari yake ya maisha ya miaka 33 aliyoitumikia hapa duniani.
Rapa huyo baba wa watoto wawili amefariki wakati akiendelea kuandaa jarida la Dk Sebi inayedaiwa kuwa aligundua dawa ya Ukimwi na kutibu wagonjwa watatu lakini alifariki katika mazingira ya kutatanisha.
Daktari huyo ambaye jina lake halisi ni Alfredo Darrington Bowman alikuwa raia wa Honduras lakini mara zote alipenda kutambuliwa kama Mwafrika anayeishi nchini Marekani.
Hussle aliyekuwa mchumba wa mwigizaji Lauren London alikuwa akiandaa jarida kuhusu kifo cha Dk Sebi akihusisha na tiba zake hasa ile inayotibu Ukimwi.
Inadaiwa kuwa Hussle aliamini kuwa kifo chake kilifanywa na wazalishaji wa dawa hasa zinazohusiana na magonjwa ya Ukimwi, kisukari na sikoseli ambayo alikuwa akiyatibu.
Dk Sebi ambaye alitumia mitishamba kutibu wagonjwa hayo, mara kadhaa alikamatwa nchini Marekani na mwaka 1987 alishtakiwa kwa kutengeneza dawa bila kuwa na kibali.
Alikamatwa zaidi ya mara mbili akiwa nchini Marekani akituhumiwa kutakatisha fedha.
Rapa Nick Cannon amesema ataendelea na utengenezaji wa jarida la Dk Sebi aliyefariki Agosti 26, 2016 akiwa katika mahabusu nchini Honduras.
Watu wengine maarufu akiwamo mbunifu wa mavazi Russel Simmons amejitolea kumsaidia Cannon katika kukamilisha kazi hiyo.
0 Comments