Na Moshy Kiyungi
Kila onyesho la bendi ya Msondo hufikia kipindi mtu akijikuta akicheka kufuatia vimbwanga vya mpulizaji wa tarumbeta Roman Mng’ande ‘Romario’ Hujituma kwa kucheza na tarumbeta huku akilitumia umbo lake fupi lililojaa minofu, kuwapagaisha watu ukumbini, vimemfanya kuwa maarufu miongoni mwa wasanii wa bendi ya Msondo Ngoma.
Majina yake kamili anaitwa Roman Mng'ande ambae ni mwanamuziki mwenye historia kubwa katika muziki hapa nchini. Umaarufu wa Romario haukuja hivi hivi bali ulitokana na mambo mbalimbali yakiwemo ya vituko, mavazi, unyoaji wake wa nywele wa aiana yake na vichekesho vingi anavyofanya akiwa kwenye kazi yake hiyo.
Msanii huyo, amevuma masikioni mwa mashabiki wengi hususan wapenzi wa muziki wa dansi hadi nje ya mipaka yetu hususan katika jiji la Nairobi ambako ni gumzo kutokana na mbwembwe zake. Licha ya kazi yake ya kupuliza tarumbeta, Romario hufanya mbwembwe lukuki zikiwemo za kuvuta kidevu chake chenye ‘mzuzu’ weye ndevu ndefu wakati akicheza jukwaani.
Aidha hufanya ‘rap’ kufokafoka huku akionesha jinsi ‘Msondo’ unavyochezwa akitumia umbo lake kubwa japo mfupi.
Mg’ande alipata elimu katika shule ya sekondari Kingurunyembe, huko Morogoro.
Alianza kuzungumzia historia yake kimuziki ambapo alisema alianza kujiingiza kwenye tasnia hiyo mwaka 1973, akiwa katika kundi la Father Kanuti, mjini Morogoro aliyekuwa mwalimu mzuri wa ala za upepo.
Alisema akiwa kwenye kundi hilo, alianza kwa kupiga vyombo mbalimbali ikiwemo tarumbeta ambalo kwa sasa ana uzoefu nalo mkubwa.
Romario alisema katika kundi hilo, alidumu kwa miaka sita, mwaka 1979 alijiunga na bendi ya Urafiki Jazz iliyokuwa na masikani yake jijini Dar es Salaam.
Kilichomsukuma yeye kujiunga na kundi la Urafiki Jazz, alisema kuwa alihitaji kukuza kipaji chake cha muziki na kujipatia ukomavu, chini ya uongozi wa bendi hiyo Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba.
Mng'ande, ambaye anasifika kwa vituko na tambo za kila aina, alisema katika kundi hilo hakuweza kudumu kwa muda mrefu kutokana na kuhitajika katika kundi la Tanzania Stars Magosi.
Alijinasibu kuwa mara kwa mara viongozi wa bendi hiyo, walikuwa wakimfuata ili aweze kujiunga nalo ili kuiongezea nguvu bendi hiyo.
Msanii huyu alisema mwaka 1981 uongozi wa Tanzania Stars Magosi, ulifanikiwa kumuhamisha kutoka bendi ya Urafiki, baada ya ‘kumpandia’ dau nono.
"Unajua sisi wasanii ni kama vile wachezaji mpira mtu akikupandia dau huwezi kuliacha, lazima umfuate...tunafanya muziki ili tupate hela sasa kama umepewa hela utaweza kuziacha….” Alisema kwa kujiamini Romario.
Aliongeza kwa kusema kuwa alipofuatwa na viongozi wa Tanzania Magosi hakuweza kukataa kwani aliangalia maslahi mbele mambo mengine baadae.
Mng’ande akiwa na bendi hiyo alifanikiwa kujiongezea umaarufu na kuanza kusikika masikioni mwa mashabiki wengi.
Hata hivyo Mng’ande alidumu katika bendi hiyo hadi mwaka 1983.
Sifa zake nzuri zilipelekea kufuatwa na viongozi wa bendi ya Juwata Jazz kipindi hicho sasa Msondo Ngoma, ili aende kujiunga na bendi hiyo.
“Viongozi wa Juwata walinitafuta na kumueleza dhamira yao ni kutaka nijiunge na bendi yao ambayo kipindi hicho ilikuwa tishio kwa bendi zingine hapa nchini” alisema Romario.
Mng’ande alisema baada ya kufuatwa na viongozi wa Juwata na kuonyesha nia ya kutaka kumchukua kwenye kundi hilo, hakufanya kosa na aliwaambia milango iko wazi.
"Lengo langu lilikuwa kuimba kwenye bendi kubwa kama Juwata, hivyo nilipofuatwa sikufanya kosa nikawaambia milango iko wazi waje tuzungumze. “alitamka Mng’ande.
Alisema mwaka 1983, akajiunga rasmi na bendi ya Juwata Jazz, wakati huo ikiwa na waimbaji mahiri akiwemo marehemu TX Moshi William, Joseph Maina, Athumani Momba, Suleiman Mbwembwe na kiongozi wa bendi hivi sasa Said Mabera na wengine wengi.
Mng'ande, alisema tokea kipindi hicho hadi sasa hajatoka kwenye bendi hiyo wala hafikirii kutoka mpaka atakapoamua kuachana na muziki.
"Kama nilirogwa basi viongozi wa Msondo walipata mganga, kwani tokea nilipojiunga na bendi hiyo hadi sasa sijatoka wala sifikirii kutoka hata iweje.
Akielezea juu ya mafanikio aliyoyapata kupitia muziki, Romario alisema “Nimepata mafanikio makubwa nikiwa katika bendi hii na imenisaidia kufahamiana na watu wengi, viongozi wa serikali, kwa kweli nimepata mafanikio makubwa katika maisha yangu…”.
Alisema kuwa hawezi kusita kukiri kwamba bendi ya Msondo, imemtoa kimaisha, amemfanya kiwango chake cha muzimki kukua siku hadi siku, hatoweza kuisahau katika maisha yake yote.
Mng'ande, alisema hana mpango wa kuanzisha bendi na lengo lake ni kuzidi kujiimarisha katika kazi yake hiyo ili bendi yake ya Msondo Ngoma, iweze kufanya vyema zaidi.
Alisema katika maisha yake ya muziki hawezi kumsahau marehemu TX Moshi kwani alikuwa rafiki yake mkubwa na alikuwa akimshauri mambo mengi.
Romario, alisema wanamuziki wengine ambao hawezi kuwasahau ni pamoja na Said Mabera na Muhidin Maalim Gurumo.
Wimbo ambao hawezi kuusahau ni kibao cha “Isikutonza iyudi Chaum”, uliotungwa na marehemu Suleiman Mwanjiro na yeye alishiriki kwa kiasi kikubwa kupiga vyombo katika wimbo huo.
“Huo wimbo ukipigwa hata niwe wapi lazima nisimame kidogo niusikilize, naupenda sana kuliko wimbo mwingine, nilishirikishwa kuupiga…” Romario alijigamba.
Alisema albamu za Msondo ambazo hawezi kuzisahau ni pamoja na ‘Mwanaume tumeumbwa mateso’ na ‘Kilio cha mtu mzima’.
Romario mbali na kipaji cha kupuliza tarumbeta, amejaaliwa kipaji cha uimbaji ambapo mara nyingi ameonekana akiimba nyimbo mbalimbali.
Romario Mng'ande ni baba wa familia yenye mke na watoto wanne.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA
0 Comments