Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume amesema uamuzi wa Mahakama Kuu kuwaengua wakurugenzi wa halmashauri kusimamia chaguzi mbalimbali nchini ni sawa na kuzuia goli la mkono katika uchaguzi.
Fatma ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Mei 24, 2019 jijini Arusha katika kongamano la taasisi ya Change Tanzania, akibainisha kuhusu hukumu hiyo ya kesi iliyofunguliwa na Bob Wangwe kwamba ina maana kubwa katika demokrasia ya Tanzania.
Hukumu hiyo ilitolewa Mei 10, 2019 na kuwaengua wakurugenzi hao wa halmashauri za majiji, miji/wilaya na manispaa kusimamia uchaguzi. Hata hivyo, Serikali imetia nia ya kukata rufaa kuhusu hukumu hiyo.
Wakurugenzi hao ambao wamekuwa wakilalamikiwa na vyama vya upinzani kuwa baadhi yao ni makada wa CCM, ndio wasimamizi wa uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kifungu cha 7(1).
Lakini, Mahakama Kuu katika hukumu yake pamoja na mambo mengine ilibatilisha kifungu hicho ikieleza kuwa kinakinzana na Katiba ya nchi Ibara za 21(1), (2) na ya 26(1), kuhusiana na ushiriki katika shughuli za uchaguzi na kutii na kufuata Katiba na sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la majaji watatu; Dk Atuganile Ngala (kiongozi wa jopo), Dk Benhajj Masoud na Firmin Matogolo kufuatia kesi ya kikatiba namba 17, ya mwaka 2018 iliyofunguliwa mahakamani hapo.
Akizungumzia hukumu hiyo leo, Fatma amesema Watanzania wengi walikuwa wanajua jinsi wakurugenzi wanavyovuruga uchaguzi lakini walikuwa kimya.
"Nimesaidia tumekwenda mahakamani tumeshinda kesi na hapa ndio tunaliondoa goli la mkono hivyo lazima tuungane" amesema.
Amesema ili kujua tatizo la wakurugenzi kusimamia uchaguzi ni vyema kutambua aliyewateua na sheria ya uchaguzi inasemaje.
"Kuna sheria ya Serikali za mitaa ambayo inazungumzia Rais kuteua wakurugenzi lakini kuna sheria ya uchaguzi ambayo inatambua hao wakurugenzi na kuwatumia.”
“Watu wanapenda kulalamika lakini hawachukui hatua ,tuige mfano wa Wangwe kwa kujitoa mhanga kufungua kesi hii,” amesema Fatma.
Kuhusu nia ya Serikali kukata rufaa, Fatma amesema kuna shinikizo la kisiasa tu na yeye kama wakili hana pingamizi kwani watakutana mahakamani.
Credit: Mwananchi
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA
0 Comments