Liverpool Yaipiga Barca Kinyama Yaitupa Nje UEFA | ZamotoHabari.

Liverpool Yaipiga Barca Kinyama Yaitupa Nje UEFA
LIVERPOOL wameonyesha kuwa wao ni wanaume wa shoka baada ya jana kuichapa Barcelona mabao 4-0 na kutinga hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Awali hakuna ambaye alikuwa anatarajia hili, lakini Liverpool wakiwa nyumbani kwao kwenye dimba la Anfi eld walionyesha kiwango cha hali ya juu sana na kufuzu kwenda fainali kwa ushindi wa 4-3.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Hispania wiki iliyopita Barcelona walipata ushindi wa mabao 3-0 na kuwa na matumaini ya kwenda fainali, lakini ghafl a kila kitu kilibadilika.

Liverpool ambao jana walimkosa mshambuliaji wao hatari Mohammed Salah ambaye ndiye kinara wa mabao kwenye timu hiyo na Ligi Kuu ya England kutokana na kusumbuliwa na majeraha walianza mchezo kwa kasi nzuri sana.


Kasi ya Liverpool iliwasaidia kupata bao la kuongoza katika dakika ya saba tu ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wao Divock Origi ambaye alifunga baada ya mabeki wa Barcelona kuzembea kuokoa mpira uliokuwa langoni mwao baada ya kugongwa kichwa kimakosa ja Jordi Alba.

Origi ameonekana kuwa muhimu sana kwa Liverpool kwa sasa kwa kuwa wikiendi iliyopita ndiye aliifungia timu hiyo bao la ushindi tena kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Newcastle waliposhinda mabao 3-2.

Baada ya bao hilo bado Liverpool waliendelea kutawala mchezo huo na kukosa nafasi kadhaa za wazi huku mwamuzi akitumia nguvu kubwa kutuliza hasira za wachezaji wa timu zote mbili kila baada ya muda mchache.

Hata hivyo, walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao hilo moja lakini waliporejea kipindi cha pili walikuwa mbogo na kupata mabao mawili ndani ya dakika mbili. Mchezaji aliyeingia kipindi cha pili mwanzoni Georginio Wijnaldum alikuwa shujaa kwenye timu hiyo baada ya kuifungia bao la pili katika dakika ya 54 na dakika mbili baadaye akafunga la tatu huku Barcelona ambayo ilikuwa inaongozwa na Lionel Messi ikiwa haina la kufanya.

Wakati Barcelona wakijiuliza bila kujua nini cha kufanya safu yao ya ulinzi iliyokuwa ikiongozwa na Gerrard Pique ilifanya tena kosa baada ya kuzembea kuokoa kona ya haraka iliyopigwa na kumkuta Origi ambaye aliifungia timu yake bao la nne katika dakika ya 76.


Sasa Liverpool ambao wameshatwaa ubingwa huo mara tano wamekwenda kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kufuzu msimu uliopita lakini wakachapwa na Real Madrid. Fainali ya mwaka huu inatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Wanda Metropolitano ambao unatumiwa na klabu ya Atletico Madrid ya nchini Hispania unaochukua mashabiki 67,000.

Sasa Liverpool wanasubiri mshindi wa leo kati ya Ajax na Tottenham Hortspur ambapo katika mchezo wa kwanza Spurs wakiwa nyumbani walilala kwa bao 1-0. Fainali ya michuano hii mikubwa zaidi barani Ulaya kwa upande wa klabu itafanyika Juni 1 mwaka huu
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini