MRADI WA MAJI WA BILIONI 1.8 WASAINIWA BUSEGA | ZamotoHabari.

Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) imesaini mkataba na Mkandarasi Kampuni ya BENNET Contractors Ltd ya Mkoani Mwanza kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa Nyashimo, Wilayani Busega Mkoani Simiyu utakaonufaisha wananchi wapatao 12,000 wa vitongoji vya Bukabile, Bulima na Mwagulanja.

Hafla ya utiaji saini ilifanyikia hivi karibuni Wilayani Busega na kushuhudiwa na wananchi, watendaji wa Serikali na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ambaye alibainisha kwamba zaidi ya asilimia 74 ya wananchi wa Busega watakua na uhakika wa maji safi na salama mara baada ya kukamilika kwa mradi.

Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga akielezea utekelezaji wa mradi huo alibainisha kuwa ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli baada ya ahadi aliyoitoa kwa wananchi wa Nyashimo ya kuwapelekea maji safi na salama.

“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alivyopita hapa Nyashimo wakati wa ziara zake aliwaahidi wananchi wa hapa kuwatatulia kero ya maji na aliiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha inatekeleza mradi haraka iwezekanavyo,” alisema Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alisema mradi utatekelezwa kwa Miezi 15 na utagharimu jumla ya Shilingi Bilioni 1.8 na kwamba unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake Mhe Mtaka alisisitiza mradi ukamilike kabla ya muda uliopangwa wa miezi 15 na alimtaka Mkandarasi kuhakikisha analifanyia kazi suala hilo na alisema endapo kama Mkandarasi atabaini urasimu katika utekelezaji wa mradi amfahamishe haraka ili kuondoa hali hiyo.

Aliongeza kuwa utekelezwaji wa mradi ni neema kwa wananchi wa Busega na aliwasihi kuchangamkia fursa zitokanazo na ujenzi wake kuanzia hatua za awali za utekelezaji na alimuagiza Mkandarasi kuhakikisha anatekeleza mradi kwa ufanisi mkubwa na kutoa kipaumbele kwa jamii inayozunguka kuwa ya kwanza kunufaika. 

Mtaka alimpongeza Mhandisi Sanga kwa jitihada zake na umahiri wa kusimamia miradi anayokabidhiwa kwa niaba ya Wizara ya Maji na alimsisitiza aendelee na moyo huo wa kizalendo na aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na wafanyakazi wa MWAUWASA.

Naye Mbunge wa Jimbo la Busega Mkoani Simiyu, Dkt. Raphael Chegeni ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi walioshuhudia tukio hilo alisema kero kubwa waliyokuwa nayo wananchi wa jimbo lake ni ukosefu wa maji safi na salama na tayari mwarobaini wake umepatikana. 

Dkt. Chegeni alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kutimiza ahadi alizotoa kwa wananchi wakiwemo wa jimbo lake na alibainisha kuwa utekelezaji wa miradi ni maelekezo ya Rais na kwamba kwa Wilaya ya Busega ipo miradi mingi inatekelezwa na aliitaja baadhi ambayo ni ya Kiloleli na Lamadi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkandarasi, Sabato Boas aliahidi kutekeleza mradi kwa muda mfupi kadri itavyowezekana na kwa utaalam unaotakiwa kuzingatia viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba. 
 Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) na Mwakilishi wa Kampuni ya BENNET Contractors Ltd, Sabato Boaz (kulia) wakisaini mkataba wa ujenzi wa Mradi wa Maji wa Nyashimo-Busega, Mkoani Simyu. Wanaoshuhudia ni viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Busega.
 Mkuu wa Mkoa Simiyu, Antony Mtaka (katikati), akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Antony Sanga mara baada ya kusaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji Nyashimo. Kulia kwa Mkuu wa Mkoa ni Mbunge wa Jimbo la Busega Mkoani Simiyu, Dkt. Raphael Chegeni.
 Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Busega, Mkoa wa Simiyu na Wajumbe wa Bodi ya MWAUWASA wakishuhudia tukio la utiaji saini mradi wa maji Nyashimo.
 Baadhi ya wananchi waliyofika kwenye hafla ya utiaji saini ujenzi wa mradi wa maji wa Nyashimo-Busega, Mkoani Simiyu wakifuatilia tukio hilo.
 Mbunge wa Jimbo la Busega Mkoani Simiyu, Dkt. Raphael Chegeni akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji wa Nyashimo- Busega.
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi MWAUWASA wakijadiliana jambo wakati wa halfa ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji wa Nyashimo. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya MWAUWASA, Edith Mudogo na Mjumbe wa Bodi, Hellen Bogohe.




Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini